NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeidhinisha rasmi mabadiliko ya jina la Habib African Bank Limited na kuanza kuitwa Africa & Gulf Bank (Tanzania) Limited, hatua inayokuja kufuatia mabadiliko katika umiliki wa hisa wa taasisi hiyo ya kifedha.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na BoT leo Juni 2,2026 mabadiliko hayo yameanza kutekelezwa rasmi kuanzia Mei 19, 2026, baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na udhibiti zinazohitajika katika sekta ya fedha nchini.
Taarifa hiyo, iliyosainiwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Sauda K. Msemo imeeleza kuwa,hatua hiyo imechukuliwa kufuatia mabadiliko ya umiliki wa hisa katika benki hiyo, jambo lililopelekea kubadilishwa kwa utambulisho wa taasisi hiyo katika soko la huduma za kifedha.
Licha ya mabadiliko ya jina, makao makuu ya benki hiyo yataendelea kubaki katika eneo lilelile lililopo katika viwanja namba 813/23 na 814/23, kwenye makutano ya Barabara za Zanaki na Indira Gandhi katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

