Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na wenzake wafikishwa mahakamani kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewafikisha mahakamani aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Essau Hossiana Ngoloka pamoja na wenzake sita wakikabiliwa na mashitaka mbalimbali ya rushwa na uhujumu uchumi yanayohusiana na matumizi mabaya ya fedha za umma katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa canteen ya halmashauri hiyo.
Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe Juni 1, 2026, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kitoki Mwakitalu ambapo walisomewa mashitaka katika mashauri matatu ya jinai ya uhujumu uchumi yenye namba ECCO 11952/2026, ECCO 11953/2026 na ECCO 11969/2026.

Mbali na Ngoloka, washtakiwa wengine ni Idrisa Mussa Naumanga, Sopharete Matete, Jerry Leonard Mwakapemba, Zacharia Cosmas Ntambala, Joachim Ibrahim Rweshunge na Jesfan Fares Ntagata.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka uliowakilishwa na Mawakili wa Serikali kutoka TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2023 wakati wakisimamia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa canteen ya Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe.

Mahakama ilielezwa kuwa,washtakiwa wanakabiliwa na kosa la kwanza la matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2022.

Inadaiwa kuwa,waliandaa na kutumia nyaraka mbalimbali za ukaguzi na tathmini ya mradi huo, kisha kuidhinisha malipo ya shilingi milioni 5.3 kwa kazi ambazo hazikuwahi kufanyika.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka, kinyume na Kifungu cha 31 cha sheria hiyo, kwa kuidhinisha malipo ya shilingi milioni 3.3 kwa fundi sanifu wa mradi huo licha ya kufahamu kuwa kazi husika haikuwa imekamilika na hivyo malipo hayo hayakuwa halali.

Shtaka la tatu linahusu madai ya kutumia risiti ya kielektroniki ya EFD ya udanganyifu yenye thamani inayozidi shilingi milioni 20, ambayo inadaiwa haikuwa imesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Mashtaka hayo yamesomwa sambamba na masharti ya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200, Marejeo ya mwaka 2022, kutokana na uzito wa tuhuma zinazowakabili washtakiwa hao.

Baada ya kusomewa mashitaka, washtakiwa wote walikana makosa yote yanayowakabili. Mahakama iliwaruhusu kuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa.

Kesi hizo zinaendeshwa na Mawakili wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, James Mosi Nyarobi na Omary Juma na zinatarajiwa kutajwa tena Juni 9, 2026 kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja za awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here