MOROGORO-Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Gerson Msigwa, ameipongeza Wizara ya Maji kwa usimamizi madhubuti wa ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda, akieleza kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati Nchini inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya maji, kilimo, nishati na uhifadhi wa mazingira nchini.
Msigwa, ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la mradi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 50.3.
Amesema kukamilika kwa bwawa hilo kutakuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za upungufu wa maji kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huku likiimarisha uwezo wa mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini inayosimamiwa na DAWASA.
“Baada ya kusuasua kwa muda mrefu tangu mwaka 1961, tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha Shilingi bilioni 336 zilizowezesha kuanza kwa mradi huu mkubwa na wa kihistoria mara baada ya kuingia madarakani. Mradi huu utanufaisha zaidi ya wananchi takriban milioni saba wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani,” amesema Msigwa.
Ameeleza kuwa mbali na kuongeza uhakika wa maji kwa wananchi, mradi huo utakuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta za kilimo, uvuvi na uzalishaji wa nishati ya umeme wa megawati 20.
Msigwa pia amefafanua Bwawa la Kidunda limezingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira na kwamba hofu zilizokuwapo awali kuhusu athari zake si za kweli.
“Maji yatakayokusanywa hapa ni lita bilioni 190. Kati ya hizo, lita bilioni mbili pekee ndizo zitakazotumika kwa siku. Zaidi ya lita milioni 600 zitaelekezwa kwenye mitambo ya DAWASA, lita milioni 400 zitahudumia mashamba ya sukari ya Mkulazi, huku zaidi ya lita milioni 900 zikiendelea kuhifadhi na kulinda ikolojia ya Mto Ruvu,” amesisitiza.

