EWURA yatangaza bei ya mafuta Juni 2026, nafuu kidogo katika Petroli

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za mafuta ya petroli nchini kuanzia Juni 3, 2026 huku zikiendelea kupanda, ikieleza kuwa hali hiyo imesababishwa kwa kiasi kikubwa na vita vinavyoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati pamoja na kuvurugika kwa usafirishaji wa mafuta duniani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA, mgogoro ulioanza Februari 28, 2026 ukizihusisha Marekani, Israel na Iran umeathiri miundombinu muhimu ya uzalishaji, uhifadhi na usafishaji wa mafuta, hali iliyosababisha kupungua kwa upatikanaji wa mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa bei za bidhaa hizo.

EWURA imeeleza kuwa,hali hiyo imechangiwa zaidi na kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.

Kufungwa kwa njia hiyo kumesababisha ongezeko la gharama za usafirishaji, bima za meli za mafuta pamoja na ucheleweshaji wa mizigo, jambo ambalo limeongeza shinikizo la bei katika soko la kimataifa.

Tanzania, ambayo huagiza sehemu kubwa ya mafuta yake kutoka Mashariki ya Kati, imeathirika moja kwa moja na mabadiliko hayo ya kimataifa.

Katika hatua ya kupunguza athari kwa wananchi na uchumi wa nchi, Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya takribani shilingi 534.91 kwa kila lita moja ya dizeli ili kusaidia kudhibiti ongezeko kubwa zaidi la bei za mafuta hayo yanayotumika katika sekta za usafirishaji, uzalishaji viwandani na huduma mbalimbali za kijamii.

Kwa mujibu wa bei mpya zilizotangazwa, mafuta ya petroli katika Jiji la Dar es Salaam yatauzwa kwa bei isiyozidi shilingi 4,086 kwa lita, huku dizeli ikiuzwa kwa shilingi 4,333 na mafuta ya taa kwa shilingi 4,685 kwa lita.

Katika Bandari ya Tanga, petroli itauzwa kwa shilingi 4,157 kwa lita, dizeli shilingi 4,404 na mafuta ya taa shilingi 4,756 kwa lita.

Kwa upande wa Mtwara, petroli itauzwa kwa shilingi 4,193 kwa lita, dizeli shilingi 4,440 na mafuta ya taa shilingi 4,792 kwa lita.
Ikumbukwe kwa mwezi Mei 2026, bei kikomo za rejareja katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zilikuwa kama ifuatavyo:

Dar es Salaam:

Petroli shilingi 4,115; Dizeli shilingi 4,248; Mafuta ya taa shilingi 4,677.

Tanga:

Petroli shilingi 4,176; Dizeli shilingi 4,309; Mafuta ya taa shilingi 4,738.

Mtwara:

Petroli shilingi 4,207; Dizeli shilingi 4,341; Mafuta ya taa shilingi 4,770.

EWURA imebainisha kuwa pamoja na changamoto za kisiasa na kiusalama katika Mashariki ya Kati, gharama za uagizaji mafuta zimeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa mafuta yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam, gharama za uagizaji zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 55.50 kwa petroli na asilimia 95.51 kwa dizeli.

Aidha, mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni yamechangia ongezeko la gharama, ambapo wastani wa kiwango cha ubadilishaji fedha kilichotumika katika ukokotoaji wa bei za mwezi Juni umeongezeka kwa asilimia 0.37.

Mamlaka hiyo imewaagiza wafanyabiashara wote wa mafuta kuzingatia bei kikomo zilizotangazwa na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka agizo hilo.

EWURA pia imewataka wamiliki wa vituo vya mafuta kuendelea kuweka wazi mabango ya bei kwa wateja na kutoa stakabadhi za kielektroniki za mauzo (EFPP) kwa kila muamala ili kuimarisha uwazi, kulinda haki za watumiaji na kusaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here