NA DIRAMAKINI
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto (WMJJWW) imesema,matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Ulinzi wa Mtoto (CPIMS) yataongeza ufanisi katika ukusanyaji wa taarifa, ufuatiliaji wa kesi za udhalilishaji na uratibu wa huduma za ulinzi wa watoto.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WMJJWW), Khatib Mwadin Khatib (wapili kushoto) akipokea Kishishkwambi cha kuhifadhia taarifa za udhalilishaji dhidi ya watoto kutoka kwa Mratibu wa Matunzo na Ulinzi wa Watoto kutoka UNICEF Tanzania, Miranda Aran Strong (wapi kulia), Ofisa Uhifadhi wa Mtoto kutoka UNICEF Zanzibar, Ahmed Rashid Ali (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi WMJJWW,Juma Ali Sima hafla ya makabidhiano imefanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa wizara hiyo.
Akizunguma Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khatibu Mwadini, wakati wa hafla ya kupokea vishikwambi 37 vilivyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF). Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa WMJJWW Kinazini Unguja.
Khatibu alisema kuwa,kwa muda mrefu changamoto kubwa ilikuwa ni ukosefu wa mfumo wa kisasa wa mawasiliano na uhifadhi wa taarifa za kesi za udhalilishaji wa watoto. Hivyo hali hiyo ilisababisha ucheleweshaji wa taarifa kufika kwa wahusika na wakati mwingine kuathiri ufanisi wa hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Alisema,matumizi ya mfumo huo yatawezesha taasisi na wadau mbalimbali kupata taarifa kwa wakati na kuchukua hatua stahiki haraka zaidi kwani uwepo wa mfumo huo pia utarahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Alifafanua kuwa,vishikwambi vilivyotolewa vitasaidia watendaji wa sekta husika kuingiza taarifa moja kwa moja kwenye mfumo na kuimarisha mawasiliano baina ya wadau.“Uhalisia wa kuwepo kwa mfumo huu unaongeza upatikanaji wa kumbukumbu na taarifa kwa wakati, jambo litakalosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa watoto wanaohitaji msaada,”alisema Khatibu.
Alisema,hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Zanzibar za kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwani kuwa mfumo wa PRIMERO unaotumika kuendesha CPIMS si jambo jipya duniani kwani tayari umetumika kwa mafanikio katika mataifa mbalimbali.
Alisema,kazi kuu ya mfumo huo ni kuhifadhi kumbukumbu za kesi, kufuatilia maendeleo yake na kuwezesha wadau kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi.Pia alibainisha kuwa,mfumo huo umezinduliwa zamani na tayari umeanza kuonesha matokeo chanya kwa kuwa baadhi ya kesi zimeshaingizwa na kufuatiliwa kupitia mfumo huo.
Alisema,taarifa zinazokusanywa zitasaidia kuonesha ukubwa wa tatizo na kuweka msingi wa maamuzi sahihi katika sekta ya ulinzi wa mtoto.
Sambamba na hilo, aliishukuru UNICEF kwa mchango wake wa vifaa na ushirikiano unaoendelea katika kuimarisha huduma za ustawi wa watoto Zanzibar.
Alisema,ushirikiano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya aina zote za ukatili na udhalilishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Wizara hiyo, Hamisa Kombo alisema,mfumo huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya wizara na UNICEF ili kujenga mfumo madhubuti wa usimamizi wa kesi Alieleza kuwa hapo awali kulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa mfumo rasmi wa kuhifadhi na kufuatilia taarifa za kesi hizo.
Hamisa alisema,kwa sasa takribani nchi 54 duniani zinatumia mfumo huo katika kuimarisha huduma za ulinzi wa mtoto. Umeongeza kusema kuwa maofisa wanaohusika tayari wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo na wameanza kuutumia katika maeneo yao ya kazi kwani lengo kuu ni kuhakikisha kila kesi inayoripotiwa inasajiliwa, inafuatiliwa na kufikishwa kwenye hatua zinazostahili kwa wakati.Naye Mratibu wa Matunzo na Ulinzi wa Watoto kutoka UNICEF Tanzania, Miranda Aran Strong alisema,shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha mifumo ya kulinda watoto.
Alisema,vishikwambi hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na uhifadhi wa taarifa za kesi za udhalilishaji pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa watoto walioathirika
Awali, Ofisa Uhifadhi wa Mtoto kutoka UNICEF Zanzibar, Ahmed Rashid Ali alisema, changamoto ya uhifadhi wa data ndiyo iliyochochea kuanzishwa kwa mfumo huo wa kidijitali.
Vifaa hivyo vitatolewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo maofisa ustawi wa jamii, Jeshi la Polisi, sekta ya afya kupitia vituo vya One Stop Center, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) pamoja na Mahakama ili kuimarisha uratibu wa huduma chini ya mfumo mmoja.


