NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua rasmi Mfumo wa Kielektroniki wa Kuoanisha Miamala (Electronic Matching System-EMS), hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi, ufanisi na ushindani katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni kati ya mabenki nchini.
Uzinduzi huo umefanywa leo Juni 8, 2026 na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wawakilishi wa mabenki mbalimbali,wadau wa sekta ya fedha pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Masoko ya Fedha Tanzania.Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Kayandabila amesema,mfumo huo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa na BoT katika kuimarisha soko la fedha za kigeni nchini, sambamba na matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya fedha.
Pia amesema,uzinduzi huo ni miongoni mwa matukio maalumu yaliyoandaliwa katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania, yatakayofanyika kuanzia Juni 12 hadi 14,mwaka huu.
“Haya ni miongoni mwa matukio muhimu ambayo yameidhinishwa na Mheshimiwa Gavana kama sehemu ya safari ya kuadhimisha miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania.Ni mwendelezo wa mageuzi yanayolenga kuifanya sekta ya fedha kuwa ya kisasa zaidi na yenye ushindani mkubwa,”amesema.
Dkt.Kayandabila ameeleza kuwa,Tanzania imepitia safari ndefu ya maboresho katika soko la fedha za kigeni tangu miaka ya 1990, huku katika miaka mitatu iliyopita kukishuhudiwa mageuzi makubwa zaidi.
Ametaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na kutungwa kwa Kanuni za Maadili ya Washiriki wa Soko la Fedha za Kigeni mwaka 2024 na maboresho ya sera mbalimbali yaliyoanza mwaka 2023.
Kwa mujibu wake, EMS itasaidia kuondoa mazingira ya ukosefu wa uwazi katika upangaji wa viwango vya ubadilishaji wa fedha kwa kuweka mfumo wa wazi na unaotegemea nguvu za soko.
“Tumefanya mageuzi makubwa katika kipindi kifupi. Mfumo huu utahakikisha viwango vya ubadilishaji wa fedha vinapatikana kwa uwazi na kwa misingi ya ushindani wa soko badala ya mazingira yasiyoonekana wazi,”amesema.Aidha, amebainisha kuwa,maboresho hayo yana umuhimu mkubwa wakati ambapo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unatarajiwa kuanza rasmi Julai Mosi mwaka huu, huku sekta ya fedha ikiwa moja ya maeneo muhimu katika kufanikisha malengo ya dira hiyo.
Mfumo utafanyaje kazi?
Akitoa maelezo ya kiufundi kuhusu mfumo huo, Mkurugenzi wa Idara ya Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro amesema,tayari kanuni za uendeshaji wa EMS zimeidhinishwa na kuchapishwa katika tovuti ya Benki Kuu.
Amesema,mfumo huo utawawezesha washiriki wa soko, wakiwemo mabenki na wauzaji wakubwa wa fedha za kigeni wanaotokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi, kufanya miamala katika mazingira ya usiri na ushindani wa haki.
“Washiriki wataweka oda zao za kununua au kuuza fedha za kigeni bila kumfahamu anayefanya muamala upande wa pili. Utambulisho wa mhusika utaonekana wakati wa hatua ya malipo baada ya muamala kukamilika,”amesema.
Kwa mujibu wa Akaro, mfumo huo utatumia kanuni ya kuoanisha oda kwa kuzingatia bei iliyowekwa na muda wa kuwasilisha oda. Ikiwa bei zinafanana, oda iliyowasilishwa kwanza ndiyo itapewa kipaumbele.
Amefafanua kuwa,EMS itatumika kwa miamala ya siku hiyo hiyo (same-day transactions) inayohusisha Shilingi ya Tanzania na Dola ya Marekani pekee, huku kiwango cha chini cha muamala kikiwa Dola za Marekani 100,000.
Soko hilo litafunguliwa saa tatu asubuhi na kufungwa saa 10 jioni kila siku za kazi.
Akaro amesema,wastani wa viwango vya ubadilishaji vitakavyopatikana wakati soko linafungwa ndiyo vitatumika kama viwango rasmi vya marejeo kwa siku inayofuata.
Pia, amesema jumla ya mabenki 32 yalishiriki maandalizi ya mfumo huo, ambapo mabenki 29 tayari yameanza kufanya miamala rasmi kupitia EMS baada ya uzinduzi huo, huku benki tatu zilizobaki zikitarajiwa kuunganishwa ndani ya wiki hii baada ya kukamilisha taratibu za mwisho.Aidha, ameeleza kuwa,Benki Kuu imeteua wawezeshaji wa soko wanane (market makers) ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha kunakuwepo ukwasi wa kutosha katika soko muda wote kwa kuweka viwango vya kununua na kuuza fedha za kigeni.
Wadau waipongeza BoT
Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Masoko ya Fedha Tanzania, Catherine Mwita amesema, uzinduzi wa EMS ni hatua ya kihistoria inayotarajiwa kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika upangaji wa bei ndani ya soko la fedha za kigeni.
“Hii ni hatua kubwa sana kwa soko letu. Tunaamini mfumo huu utaongeza uwazi, kuimarisha ushindani na kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika masuala ya bei,” amesema.
Ameahidi kuwa,jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Benki Kuu pamoja na mabenki ya biashara ili kuhakikisha washiriki wote wanazingatia kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wawezeshaji wa Soko, Aziz Chacha amesema EMS imezinduliwa wakati muafaka kutokana na hali ya ukwasi iliyopo katika soko la fedha za kigeni nchini.
Amesema,wawezeshaji wa soko watahakikisha wanazingatia kikamilifu masharti na miongozo yote iliyowekwa ili kufanikisha malengo ya mfumo huo.
Uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuoanisha Miamala ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea kuwa na soko la fedha la kisasa, lenye uwazi na ushindani unaokidhi viwango vya kimataifa.
Vilevile mfumo huo utaongeza ufanisi katika biashara ya fedha za kigeni, kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi za soko na kuongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa taifa katika kipindi kijacho.





