NA DIRAMAKINI
Timu ya Taifa ya Norway imeanza vyema kampeni yake ya michuano ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Iraq katika mchezo wa Kundi I uliochezwa jana Boston Stadium, Foxborough nchini Marekani.
Mshambuliaji nyota Erling Haaland kupitia mtanange huo ameandika historia kwa kufunga mabao yake mawili ya kwanza kabisa katika fainali za Kombe la Dunia.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Norway ilionesha ubora wake tangu dakika za mwanzo na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 29 kupitia Haaland, ambaye alitumia vyema nafasi aliyopata na kuiweka timu yake mbele.
Iraq ilijitahidi kusawazisha na kufanikiwa kupata bao dakika ya 39 kupitia Hussein, lililorejesha matumaini kwa mashabiki wa taifa hilo.
Hata hivyo, furaha yao haikudumu kwa muda mrefu baada ya Haaland kufunga bao lake la pili dakika ya 43 na kuipa Norway uongozi wa mabao 2-1 kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kilishuhudia Norway ikiendelea kutawala mchezo na kuongeza presha kwa wapinzani wake.
Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 76 wakati beki Leo Østigård alipofunga bao la tatu na kuifanya Iraq kuwa katika hali ngumu ya kurejea mchezoni.
Katika dakika za nyongeza, Norway ilihitimisha ushindi wake kwa bao la nne lililotokana na kujifunga kwa Hussein wa Iraq katika dakika ya 90+6, na kuifanya mechi kumalizika kwa ushindi wa mabao 4-1 kwa upande wa Norway.
Matokeo hayo yanaiwezesha Norway kushika nafasi ya kwanza katika Kundi I ikiwa na alama tatu baada ya kucheza mechi moja.
Ufaransa pia imeanza kwa ushindi na kushika nafasi ya pili kwa alama tatu, huku Norway ikiongoza kutokana na tofauti ya mabao.
Senegal inashika nafasi ya tatu bila alama yoyote, wakati Iraq inabakia mkiani mwa kundi hilo baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza.
Mbali na ushindi huo muhimu, macho mengi yalielekezwa kwa Haaland ambaye kwa mara ya kwanza amefunga mabao katika hatua za fainali za Kombe la Dunia.
Mabao hayo mawili yanamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuwa tishio kubwa kwa mabeki wa timu pinzani kadri michuano hiyo inavyoendelea.
Aidha,kwa ushindi huo, Norway imepeleka ujumbe kwa wapinzani wake kwamba ipo tayari kupambana kwa nguvu katika harakati za kutafuta nafasi ya kufuzu hatua inayofuata ya michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.
Wakati huo huo, Iraq italazimika kujipanga upya katika michezo ijayo ili kufufua matumaini ya kusalia kwenye mbio za kufuzu kutoka Kundi I.
