NA DIRAMAKINI
TIMU ya Taifa ya Uswisi imeonesha njia ya kusonga mbele katika Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Timu ya Taifa ya Bosnia and Herzegovina mabao 4-1.
Mtanange huo wa Kundi B umepigwa Juni 18,2026 katika Dimba la SoFi (Los Angeles Stadium) jijini California nchini Marekani.
Katika mchezo huo wa raundi ya pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la FIFA 2026, pande zote zilionekana kutoshana nguvu hadi dakika ya 74 ndipo Uswisi ikapata bao la kwanza kupitia kwa Johan Manzambi.
Wakati mambo yakionekana kuwanyookea Uswisi, kwa Bosnia and Herzegovina mambo yalikuwa shubiri baada ya dakika ya 80',Tarik Muharemovic kupigwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha Breel Embolo.
Uchache wa Wabosnia uwanjani ulionekana kuwakatisha tamaa katika mapambano kwani, dakika ya 85',Ruben Vargas aliipatia tena Timu ya Taifa ya Uswisi bao la pili.
Dakika ya 90', Manzambi alirejea tena nyavuni kwa bao safi ambalo lilizidisha maumivu zaidi, kabla ya dakika 90+3', Ermin Mahmic kuwafuta machozi Wabosnia kwa bao pekee ambalo, hata hivyo halikuwa na nguvu.
Aidha,dakika ya 90+7', kupitia mkwaju wa Penalti,Granit Xhaka aliipatia Uswisi bao la nne ambalo hadi mtanange huo unatamatika ubao ulikuwa unasoma Uswisi mabao 4 huku Bosnia and Herzegovina ikiwa na bao 1.
