NA GODFREY NNKO
MIFUKO mitano ya uwekezaji inayosimamiwa na kampuni ya iTrust Finance Ltd imefikia thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 550 ndani ya kipindi cha miezi 16 tangu kuanzishwa kwake, hatua inayoashiria kuongezeka kwa mwamko wa uwekezaji miongoni mwa Watanzania pamoja na imani yao katika mifumo rasmi ya uwekezaji wa pamoja.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wa kwanza wa mifuko hiyo uliofanyika leo Juni 20,2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa iTrust Finance Ltd, Profesa Mohamed Warsame amesema mifuko hiyo ilianza shughuli zake mwezi Desemba 2024 ikiwa na mtaji wa shilingi bilioni 50, lakini sasa imefikia shilingi bilioni 550, sawa na ukuaji wa zaidi ya mara 10 ndani ya mwaka mmoja na nusu.
Amesema,mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa Watanzania wameanza kutambua umuhimu wa uwekezaji kama njia ya kujenga ustawi wa kifedha na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
“Tulianza na shilingi bilioni 50 mwezi Desemba 2024 na leo tumevuka shilingi bilioni 550. Ukuaji huu wa zaidi ya mara 10 ndani ya kipindi kifupi ni ishara kuwa Watanzania wako tayari kuwekeza kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe,”amesema Profesa Warsame.
Mifuko hiyo inayosimamiwa na iTrust ni pamoja na iCASH Fund, iSAVE Fund, iINCOME Fund, iGROWTH Fund na IMAAN Fund ambayo imeendelea kuvutia wawekezaji kutoka makundi mbalimbali ya jamii.
Kwa mujibu wa Profesa Warsame, vijana wamekuwa miongoni mwa kundi linaloongoza kwa ushiriki katika uwekezaji kupitia mifuko hiyo, jambo ambalo limetokana kwa kiasi kikubwa na matumizi ya teknolojia ya kidigitali kupitia programu maalumu ya kampuni hiyo.
“Tumefarijika kuona vijana wamekuwa mstari wa mbele katika uwekezaji. Kupitia mfumo wetu wa kidigitali, tumeona kuwa sehemu kubwa ya wawekezaji wanaofanya uwekezaji kila siku ni vijana. Hii inaonesha mwamko mkubwa wa kizazi hicho katika kujenga mustakabali wao wa kifedha,”amesema.
Mkutano huo mkuu wa mwaka wa 2025 umewakutanisha wanahisa na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi, ambapo baadhi wameshiriki ana kwa ana katika Ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam huku wengine wakifuatilia kwa njia ya mtandao.
Katika mkutano huo, wawekezaji wamepata fursa ya kupitia taarifa za utendaji wa mifuko, kusikiliza ripoti za wadhamini na wakaguzi wa hesabu, kujadiliana na menejimenti pamoja na kupiga kura kuhusu maamuzi mbalimbali ya kimkakati yanayolenga kuimarisha utendaji wa mifuko hiyo.
Profesa Warsame amesema, fedha zinazowekezwa kupitia mifuko hiyo zimeelekezwa katika vyombo mbalimbali vya uwekezaji ikiwemo hisa za kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hati fungani za serikali na taasisi za kifedha pamoja na uwekezaji mwingine wenye tija.
Pia,ameeleza kuwa,faida yote inayopatikana kutokana na uwekezaji huo hugawanywa kwa wanahisa kulingana na mchango wao, jambo ambalo limewawezesha kuona matokeo halisi ya uwekezaji wao.
“Wanahisa wameweza kuona mafanikio ya uwekezaji wao na namna ambavyo fedha zao zimezalisha mapato. Hii ni hatua muhimu katika kujenga imani kwa wawekezaji na kuhamasisha ushiriki zaidi wa wananchi katika soko la mitaji."
Akifafanua kuhusu mifuko hiyo, amesema iCASH Fund inalenga uwekezaji katika hati fungani za muda mfupi na kuwapa wawekezaji wastani wa faida ya takribani asilimia 12 kwa mwaka.
Kwa upande wa iSAVE Fund na iINCOME Fund, amesema,mifuko hiyo inawekeza zaidi katika hati fungani za muda mrefu ambapo wawekezaji wamekuwa wakipata wastani wa faida ya asilimia 13.5 kwa mwaka.
Ameongeza kuwa,IMAAN Fund, unaofuata misingi ya uwekezaji unaozingatia maadili na sheria za Kiislamu, umefanikiwa kupata faida ya zaidi ya asilimia 45, huku iGROWTH Fund ukiwa mfuko uliofanya vizuri zaidi kwa kurekodi ukuaji wa zaidi ya asilimia 114 kutokana na uwekezaji wake katika soko la hisa.
Kwa mujibu wake, mafanikio hayo yanaonesha kuwa mifuko hiyo imekuwa chombo muhimu kwa Watanzania wanaotafuta njia salama na zenye tija za kukuza mitaji yao.
Profesa Warsame amewashukuru wawekezaji wote walioweka imani yao katika mifuko hiyo na kuwataka Watanzania wengi zaidi kutumia fursa zilizopo katika soko la mitaji ili kujenga ustawi wa kifedha wa muda mrefu.
Hata hivyo, amebainisha kuwa moja ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu uwekezaji wa pamoja kutokana na soko la mitaji nchini kuwa bado changa.
Amesema,kampuni hiyo itaendelea kutoa elimu na hamasa kwa umma ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.
Naye Mhasibu wa Mifuko ya iTrust, Francis Samkyi amesema,ukuaji mkubwa uliorekodiwa na mifuko hiyo unaonesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu fursa za uwekezaji pamoja na kuimarika kwa imani katika mifumo rasmi ya uwekezaji inayodhibitiwa na mamlaka husika.
Amesema,mkutano huo pia umethibitisha dhamira ya iTrust katika kuzingatia uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wawekezaji, mambo ambayo yameendelea kuwa msingi muhimu wa kuvutia wawekezaji katika bidhaa za uwekezaji zilizo chini ya usimamizi wa kitaalamu.
Miongoni mwa ajenda muhimu zilizojadiliwa katika mkutano huo ni mapendekezo ya kufanya marekebisho ya nyaraka za uendeshaji wa mifuko (Trust Deeds) kwa lengo la kuimarisha mifumo ya utawala bora, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kupanua fursa za uwekezaji kulingana na mabadiliko ya soko.
Moja ya mapendekezo makubwa yaliyowasilishwa ni kuruhusu iGROWTH Fund kuwekeza katika Exchange Traded Funds (ETFs), hatua inayotarajiwa kuongeza wigo wa uwekezaji na kuimarisha uwezo wa mfuko huo kuzalisha mapato kwa wawekezaji.
Kwa upande wa IMAAN Fund, wawekezaji wamejadili marekebisho yatakayopanua maeneo ya uwekezaji yanayokubalika kwa kuzingatia sera za mfuko huo na misingi yake ya kimaadili.
Aidha,mkutano huo umeweka alama muhimu katika maendeleo ya sekta ya uwekezaji wa pamoja nchini Tanzania, huku ukuaji wa mifuko ya iTrust ukiendelea kuonyesha nafasi kubwa ya soko la mitaji katika kuchochea ujenzi wa utajiri wa muda mrefu kwa wananchi.
iTrust Finance Limited ni kampuni yenye leseni ya kutoa huduma za kifedha, inayodhibitiwa na
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana
(CMSA).
Kampuni imepewa leseni za kufanya shughuli za udalali wa hisa, usimamizi wa mifuko ya uwekezaji na ushauri wa uwekezaji, ikitoa suluhisho bunifu za uwekezaji zinazochochea ujumuishaji wa kifedha na kusaidia watu binafsi pamoja na taasisi kujenga utajiri
wa muda mrefu.




