NA DIRAMAKINI
MKAGUZI wa Polisi wa Kata ya Mwabusalu wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu,Bundala Elias amefanya ziara ya kipekee katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo kwa kutumia ngamia, akilenga kuhamasisha wananchi kuendelea kulinda na kudumisha amani,utulivu na usalama katika jamii.
Ziara hiyo iliyofanyika Juni 7, 2026 katika Kijiji cha Bukundi, Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, ilikuwa sehemu ya kampeni ya Jeshi la Polisi ya kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola katika kuzuia na kupambana na vitendo vya uhalifu.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika kijiji hicho, Mkaguzi Bundala alisema kuwa,amani na usalama ni nguzo muhimu za maendeleo ya jamii yoyote, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuzilinda na kuzidumisha.
Alieleza kuwa,Jeshi la Polisi linaendelea kutegemea ushirikiano wa wananchi katika kupata taarifa za uhalifu na wahalifu, jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa katika kudhibiti matukio mbalimbali ya kihalifu katika maeneo mengi nchini.
“Wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu au watu wanaojihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa jamii. Ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu."
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuwa waangalifu na matumizi ya mitandao ya kijamii, akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia majukwaa hayo kwa kuandika, kusambaza au kuchapisha maudhui yenye lugha za matusi,uchochezi au zisizo na staha dhidi ya viongozi na watu wengine.
Alisisitiza kuwa,matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanaweza kusababisha migogoro, kuvuruga mshikamano wa kijamii na hata kuhatarisha amani iliyopo, hivyo ni muhimu kwa watumiaji wa mitandao hiyo kuzingatia sheria, maadili na wajibu wao katika kutoa maoni au kusambaza taarifa.
“Uhuru wa kutoa maoni unaambatana na wajibu wa kuheshimu sheria na haki za wengine. Tunawasihi wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya zinazochochea maendeleo na mshikamano wa jamii badala ya kueneza chuki au maneno yanayoweza kuvuruga amani."
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walieleza kufurahishwa na njia iliyotumiwa na mkaguzi huyo kufikisha ujumbe kwa jamii, wakisema matumizi ya ngamia yamevutia wananchi wengi kujitokeza na kusikiliza maelekezo ya usalama na amani.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mbinu za polisi za kuendelea kuwafikia wananchi kwa njia mbalimbali ili kuongeza uelewa kuhusu masuala ya usalama, kuimarisha ulinzi shirikishi na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza kuwa, mafanikio katika kudhibiti uhalifu yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, viongozi wa serikali za mitaa na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuhakikisha mazingira ya amani na utulivu yanaendelea kuwepo kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.
