NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Brazil iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi mkubwa wa miundombinu ya maji unaofahamika kama Ceará Water Belt (Ukanda wa Maji wa Ceará), ambao umeelezwa na wataalamu kama “mto bandia” wenye urefu wa takribani kilomita 145.
Mradi huo unalenga kupeleka maji katika baadhi ya maeneo makavu zaidi ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, huku ukitarajiwa kukamilika rasmi mwezi Juni,mwaka 2026.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za rasilimali za maji za jimbo la Ceará, mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji wake, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa katika juhudi za Brazil za kukabiliana na changamoto za ukame, upungufu wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mradi wa Ceará Water Belt umeundwa kusafirisha maji kutoka Mto São Francisco kwenda maeneo ya ndani ya jimbo la Ceará ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikumbwa na ukame wa mara kwa mara.
Aidha,mfumo huo unahusisha mifereji mikubwa ya wazi, vichuguu na njia maalumu za kupitisha maji kwa kutumia nguvu ya mvuto wa asili badala ya kutegemea pampu kwa kiwango kikubwa.
Maji hayo yataanzia katika Bwawa la Jati na kusafirishwa hadi maeneo ya Nova Olinda na vyanzo vya Mto Cariús, jambo litakaloongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi na shughuli za kiuchumi katika eneo la Cariri, ambalo ni mojawapo ya vituo muhimu vya maendeleo katika jimbo hilo.
Wataalamu wa miundombinu wanaeleza kuwa, matumizi ya mfumo wa mvuto wa asili yatapunguza gharama za uendeshaji kwa muda mrefu na kufanya mradi huo kuwa endelevu zaidi ikilinganishwa na miradi inayotegemea matumizi makubwa ya nishati ya kusukuma maji.
Jimbo la Ceará linapatikana katika eneo la sertão, ambalo ni moja ya maeneo yenye ukame mkubwa nchini Brazil. Mvua katika eneo hilo huwa chache na zisizo na uhakika, hali inayosababisha changamoto kwa wakazi, sekta ya kilimo na maendeleo ya viwanda.
Kwa miaka mingi, serikali za mitaa na shirikisho zimekuwa zikitafuta mbinu za kuunganisha vyanzo vya maji ili kupunguza utegemezi wa mabwawa na visima vya ndani vinavyoathiriwa kwa urahisi na vipindi virefu vya ukame. Mradi wa Ceará Water Belt umeonekana kuwa sehemu muhimu ya mkakati huo wa muda mrefu.
Mara baada ya kukamilika, mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha moja kwa moja takribani wananchi 561,000 katika manispaa 24.
Aidha, kwa kuunganishwa na mifumo mingine ya usambazaji maji, mradi huo unaweza kufikia zaidi ya watu milioni tano katika eneo kubwa la Ceará, ikiwemo maeneo ya mji mkuu wa jimbo hilo.
Mamlaka zimeeleza kuwa kipaumbele kikuu kitakuwa ni kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu kabla ya kuelekeza huduma hiyo katika sekta nyingine kama viwanda, utalii, ufugaji na kilimo cha umwagiliaji.
Serikali ya Ceará kwa kushirikiana na Serikali ya Shirikisho la Brazil imewekeza takribani dola za Marekani milioni 159 katika utekelezaji wa mradi huo, ingawa baadhi ya sehemu za mwisho za ujenzi zimeongeza gharama kutokana na ugumu wa kazi za kihandisi zinazohitajika.
Mbali na manufaa ya muda mrefu ya usalama wa maji, mradi huo pia umekuwa chanzo cha ajira kwa maelfu ya wananchi.
Zaidi ya wafanyakazi 1,500 na mamia ya mashine nzito zimehusishwa katika shughuli za ujenzi, jambo lililochochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na mradi huo.
Wachambuzi wa mazingira wanaona mradi wa Ceará Water Belt kama mfano wa jinsi mataifa yanavyoanza kutumia miradi mikubwa ya miundombinu kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Kadiri vipindi vya ukame vinavyozidi kuwa virefu na visivyotabirika, upatikanaji wa maji safi umeendelea kuwa suala nyeti kwa mamilioni ya watu duniani.
Kwa Brazil, mto huo si tu mradi wa ujenzi wa mifereji ya maji, bali ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kulinda maisha ya wananchi, kuimarisha uzalishaji wa kiuchumi na kuongeza ustahimilivu dhidi ya majanga ya ukame katika miongo ijayo. (okdiario.com)
