NA DIRAMAKINI
RAIS wa Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF), Fouzi Lekjaa, ametangaza kuwa nchi hiyo haitawasilisha tena maombi ya kuandaa mashindano ya soka ya Afrika chini ya mwavuli wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hatua inayotafsiriwa kama mabadiliko makubwa katika mkakati wa taifa hilo ndani ya soka la bara hilo.
Akizungumza katika mahojiano na Al Jazeera 360, Lekjaa amesema kuwa,kuanzia sasa Morocco haitawania tena haki ya kuandaa mashindano yoyote ya Afrika bila kujali ukubwa au aina yake.
“Kuanzia leo, Morocco haitawasilisha tena maombi yoyote ya kuandaa mashindano ya Afrika, bila kujali aina yake. Nchi nyingine zikihitaji kuyaandaa, tunawatakia kila la heri,” amesema Lekjaa.
Tangazo hilo limeibua mjadala mkubwa ndani ya familia ya soka la Afrika kutokana na nafasi muhimu ambayo Morocco imekuwa nayo katika miaka ya hivi karibuni.
Taifa hilo limekuwa miongoni mwa nchi zilizobeba jukumu kubwa la kuandaa mashindano mbalimbali ya CAF na hata kutoa viwanja kwa mataifa mengine ambayo hayakuwa na miundombinu inayokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, Morocco imewekeza mabilioni ya dola katika ujenzi wa viwanja vya kisasa, vituo vya mazoezi, hoteli na miundombinu mingine ya michezo, jambo lililoifanya kuwa moja ya vituo vikuu vya soka barani Afrika.
Nchi hiyo pia imekuwa mwenyeji wa michuano mikubwa ya CAF na imejijengea sifa ya kuwa mbadala wa haraka pale nchi nyingine zinaposhindwa kutimiza masharti ya kuandaa mashindano.
MALALAMIKO NA TUHUMA NDIZO CHANZO?
Kwa mujibu wa Lekjaa, moja ya sababu zilizochangia uamuzi huo ni malalamiko ya mara kwa mara na tuhuma kwamba Morocco imekuwa ikipewa upendeleo ndani ya mfumo wa soka la Afrika.
Katika mahojiano hayo, amesisitiza kuwa kile ambacho baadhi ya watu wanakiita “upendeleo” si kingine bali ni utayari wa Morocco kuchukua jukumu la kuandaa mashindano ambayo mara nyingi hayapati waandaaji kutoka mataifa mengine.
Tamko hilo pia linakuja miezi michache baada ya kumalizika kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025/26 lililoandaliwa nchini Morocco na ambalo lilighubikwa na mvutano mkubwa kufuatia fainali yenye utata kati ya Morocco na Senegal.
Sakata hilo liliibua mjadala mpana kuhusu usimamizi wa mashindano na nafasi ya viongozi wa Morocco ndani ya CAF.
Wachambuzi wa michezo wanaamini kuwa, uamuzi huo pia unaendana na mkakati mpya wa Morocco wa kuelekeza nguvu zake katika matukio makubwa ya kimataifa.
Kwa sasa Morocco ipo katika maandalizi makubwa ya kuandaa Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2030 kwa ushirikiano na mataifa ya Hispania na Ureno.
Aidha, taifa hilo limepewa majukumu ya kuandaa matukio mengine makubwa ya kimataifa ya soka katika miaka ijayo.
Katika miaka ya karibuni, Morocco imejijengea hadhi ya kuwa moja ya mataifa yenye ushawishi mkubwa zaidi katika diplomasia ya michezo barani Afrika, huku soka likitumika kama nyenzo muhimu ya kuimarisha mahusiano yake ya kimataifa.
Iwapo msimamo huo utadumu kwa muda mrefu, CAF inaweza kukabiliwa na changamoto ya kupata waandaaji wa haraka wa mashindano yake makubwa, hasa ikizingatiwa kwamba Morocco imekuwa ikichukua jukumu hilo mara kwa mara wakati mataifa mengine yanaposhindwa kukidhi masharti ya uandaaji.
Kwa upande mwingine, hatua hiyo inaweza kufungua fursa kwa mataifa mengine ya Afrika kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya michezo na kuwania kuandaa mashindano ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakihusishwa na Morocco.
Aidha,tangazo la Fouzi Lekjaa linaashiria mwisho wa enzi muhimu katika historia ya soka la Afrika, ambapo Morocco imekuwa kitovu kikuu cha maandalizi na uandaaji wa mashindano ya bara hilo.
Hata hivyo, wakati taifa hilo likielekeza macho yake kwenye matukio makubwa ya kimataifa kama Kombe la Dunia 2030, maswali yanaendelea kubaki kuhusu nani atakayechukua nafasi yake katika kuhakikisha mashindano ya CAF yanaendelea kupata waandaaji wenye uwezo na miundombinu ya kisasa.
