Mtaalamu wa usalama wa mtandao,Yusuph Kileo asisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi katika enzi za Akili Unde (AI)

NA DIRAMAKINI

MTAALAMU wa Masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo amesema, kuimarisha usalama wa mtandao ni msingi muhimu wa kulinda taarifa binafsi za wananchi na kujenga imani katika mifumo ya kidijitali huku dunia ikiendelea kushuhudia kasi ya matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence-AI) na teknolojia zinazoibukia.
Kileo ametoa kauli hiyo aliposhiriki kama mchangiaji katika jopo la wataalamu kwenye 𝐊𝐨𝐧𝐠𝐚𝐦𝐚𝐧𝐨 𝐥𝐚 𝐊𝐰𝐚𝐧𝐳𝐚 𝐥𝐚 𝐌𝐰𝐚𝐤𝐚 𝐥𝐚 𝐅𝐚𝐫𝐚𝐠𝐡𝐚 𝐧𝐚 𝐔𝐥𝐢𝐧𝐳𝐢 𝐰𝐚 𝐓𝐚𝐚𝐫𝐢𝐟𝐚 𝐁𝐢𝐧𝐚𝐟𝐬𝐢 𝐓𝐚𝐧𝐳𝐚𝐧𝐢𝐚 𝟐𝟎𝟐𝟔 lililofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo mada kuu ilikuwa "Kuimarisha Usalama wa Mtandao ili Kulinda Taarifa Binafsi katika Enzi ya Akili Unde na Teknolojia Zinazoibukia."

Akizungumza katika mjadala huo, Kileo amesema,mabadiliko ya kidijitali yanayoendelea katika sekta za serikali, biashara na jamii yamefungua fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi na utoaji wa huduma bora, lakini pia yameongeza hatari za mashambulizi ya mtandao na ukiukwaji wa faragha za wananchi.

Amebainisha kuwa,matumizi ya teknolojia kama akili unde, huduma za kompyuta mtandaoni (cloud computing), huduma za kifedha kidijitali, mifumo ya utambulisho wa kidijitali na vifaa vinavyounganishwa kupitia intaneti yameleta mapinduzi makubwa, lakini yanahitaji mifumo madhubuti ya usalama ili kulinda taarifa za watumiaji.
Katika mjadala huo, washiriki walijadili namna ambavyo serikali, mamlaka za udhibiti, vyombo vya kutekeleza sheria, watoa huduma za teknolojia pamoja na wataalamu wa usalama wa mtandao wanaweza kushirikiana kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya mtandao, kuongeza ulinzi wa taarifa binafsi na kujenga mifumo ya kidijitali inayotegemewa na wananchi.

Aidha,Kileo amesema,ushirikiano wa wadau mbalimbali ni nguzo muhimu katika kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanaenda sambamba na usalama wa taarifa, huku yakichochea ubunifu, ukuaji wa uchumi na ujumuishaji wa kidijitali bila kuhatarisha haki za watumiaji.
Pia,ameeleza kuwa,wakati dunia ikiendelea kukumbatia teknolojia mpya, ni muhimu kuweka mikakati ya kudhibiti vihatarishi vya mtandao, kuimarisha mifumo ya ulinzi wa taarifa na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu usalama wa kidijitali.

Amesema,mjadala huo umeibua mapendekezo mbalimbali ya kitaalamu kuhusu namna ya kulinda taarifa binafsi huku ukiendelea kuunga mkono ubunifu wa teknolojia, ukuaji wa uchumi wa kidijitali na upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa makundi yote ya jamii.
Mkutano huo umekutanisha wataalamu wa usalama wa mtandao, watunga sera, wadhibiti wa sekta mbalimbali, wawakilishi wa vyombo vya dola, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa teknolojia kujadili mustakabali wa ulinzi wa taarifa binafsi nchini Tanzania katika kipindi ambacho matumizi ya teknolojia yanaendelea kukua kwa kasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here