ARUSHA-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. James Millya amekuwa Mgeni Rasmi kwenye hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshima ya washiriki wa warsha ya Nne ya Kimataifa ya Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Uendeshaji (Fourth WMO International Workshop on Operational Climate Prediction-OCP4) iliyofanyika Juni 29, 2026 jijini Arusha.
Akiwakaribisha washiriki katika chakula hicho, Mhe. Millya aliwambia kuwa Tanzania ni nchi ya Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Zanzibar na la muhimu zaidi ni nchi yenye amani, hivyo aliwakaribisha kutembelea vivutio vya utalii bila hofu ya maisha na mali zao.Hafla hiyo ya chakula cha jioni, Mhe. Naibu Waziri amesema inawakumbusha kuwa ushirikiano wa wadau duniani haujengwi tu kupitia hafla rasmi bali hafla kama hizo pia zina nafasi kubwa ya wadau kubadilishana mawazo, uzoefu na kujenga urafiki kwa manufaa ya wote.
Naibu Waziri Millya alisema,Tanzania ni nchi ya utamaduni mwingi na kwamba wageni walipowasili nchini, walipatiwa shuka la kimasai ambalo kwa utamaduni wa kimasai shuka hilo sio nguo tu, bali ni alama ya utambulisho, ustahamilivu na asili."Shuka hili linawakilisha urithi wa kujivunia wa kabila la kimasai ambalo asili yao ni mkoa huu wa Arusha na kujipatia shuka hilo ni ukumbusho wa ujio wenu hapa nchini Tanzania,"Mhe.Millya alisema.
Mhe. Millya aliwapongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) chini ya Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Ladislaus Chang'a na wadau wengine kwa kuratibu uenyeji wa Tanzania wa warsha hiyo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika na Tanzania kuwa muasisi.











