NA DIRAMAKINI
MTUMISHI wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika, Respicius Speratus Mushobozi ambaye ni Mhandisi wa Rasilimali Maji kutoka Wizara ya Maji amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma akikabiliwa na tuhuma mbalimbali zinazohusisha rushwa,uhujumu uchumi, ubadhirifu wa fedha za umma na kughushi nyaraka.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye namba ECO:12956/2026 inayomkabili Mushobozi dhidi ya Jamhuri ilifunguliwa Juni 10, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma,Mheshimiwa Eva Mushi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anatuhumiwa kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake pamoja na kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za umma kiasi cha shilingi milioni 72 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ya usimikaji wa vigingi na ukaguzi wa birika za maji katika Mkoa wa Tabora.
Vitendo hivyo vinadaiwa kufanyika kinyume na masharti ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2022, pamoja na vifungu mbalimbali vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200, Marejeo ya mwaka 2022.
Mbali na makosa hayo, Mushobozi pia anakabiliwa na mashitaka ya kughushi nyaraka, kosa ambalo linadaiwa kufanyika kinyume na vifungu vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022.
Inadaiwa kuwa,nyaraka hizo zilitengenezwa au kutumika kwa namna iliyolenga kuhalalisha malipo au matumizi ya fedha zinazohusishwa na mradi husika.
Hata hivyo, wakati shauri hilo lilipotajwa mahakamani, mshtakiwa alikana mashitaka yote yaliyosomwa mbele ya mahakama.
Aidha,baada ya kusikiliza maombi ya pande zote, mahakama ilimruhusu kuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa.
Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Juni 25, 2026, litakapokuja tena kwa ajili ya hatua nyingine.
