NA DIRAMAKINI
WATUMISHI saba wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni pamoja na mzabuni mmoja wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Manyoni wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, kuongoza genge la uhalifu, ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 501.
Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 13485/2026 imefunguliwa Juni 16,2026 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni,Mheshimiwa Ailisile Mwankejela.
Washtakiwa katika shauri hilo ni aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, George Mzeru, pamoja na maafisa mahesabu Emilian Mauki, Lutufyo Mwakapala, Edward Kilumbu, Revania Ruheta, Doreen Shirima na Salum Mafita.
Mshitakiwa mwingine ni mzabuni wa kampuni ya ML Kimboka General Trading, Michael Mushi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani na Wakili wa Serikali, Godfrey Songolo, washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya makosa sita yanayohusiana na matumizi mabaya ya fedha za umma na uhalifu wa kiuchumi.
Makosa hayo yanajumuisha utakatishaji fedha, kuongoza genge la uhalifu, kuisababishia mamlaka husika hasara, wizi unaofanywa na watumishi wa umma, ufujaji wa mali na ubadhirifu wa rasilimali za umma.
Upande wa mashtaka unadai kuwa,kati ya Julai 1,2024 na Mei 29,2026, washtakiwa hao kwa pamoja walijihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu wa kiuchumi vilivyosababisha hasara kubwa kwa Serikali.
Miongoni mwa tuhuma zinazowakabili ni kuhamisha, kutumia au kuficha fedha zinazodaiwa kupatikana kwa njia zisizo halali pamoja na kushiriki katika mtandao wa uhalifu uliolenga kupoteza fedha za umma.
Kwa mujibu wa sheria, makosa ya utakatishaji fedha yanachukuliwa kuwa miongoni mwa makosa makubwa ya kiuchumi kutokana na athari zake katika mfumo wa fedha na uchumi wa taifa.
Vilevile, kosa la kuisababishia Serikali hasara na ubadhirifu wa mali za umma ni miongoni mwa makosa yanayopewa uzito mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote, hata hivyo wamekosa dhamana kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi Juni 30, 2026 kwa ajili ya kutajwa kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea.
