Rais Dkt.Samia ayataka mashirika ya umma kujitegemea,apokea gawio la shilingi trilioni 1.327

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika na taasisi za umma nchini kuweka mikakati madhubuti ya kujiendesha kwa ufanisi, kuongeza tija na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini ili yaweze kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo pamoja na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango ya Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.
Rais Dkt.Samia ametoa maelekezo hayo leo Juni 30,2026 wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka mashirika ya umma iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema,ni muhimu kwa mashirika ambayo bado hayajaanza kutoa gawio kwa Serikali kujitathmini, kubaini changamoto zinazowakabili na kujifunza kutoka kwa taasisi zinazofanya vizuri ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji na mchango wao katika mapato ya Serikali.

“Hatutoweza kujenga uchumi wenye ushindani kwa kuwa na taasisi zinazofanya kazi kwa mazoea.Tunapoelekea kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni lazima taasisi zetu zipimwe kwa matokeo na si kwa takwimu pekee.Huo ndiyo mwelekeo wa taifa letu."

Katika hafla hiyo, Rais Dkt.Samia amepokea jumla ya shilingi trilioni 1.327 kama gawio na michango kutoka mashirika ya umma yaliyo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.

Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka 2025, ambapo Serikali ilipokea shilingi trilioni 1.028.
Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema, mashirika na kampuni za kibiashara zimechangia shilingi bilioni 800 sawa na asilimia 60 ya makusanyo yote.

Pia amesema,taasisi mbalimbali zimechangia shilingi bilioni 406 kupitia mapato ghafi, kiasi kinachowakilisha asilimia 30 ya makusanyo yote, huku mapato mengine yakichangia shilingi bilioni 121, sawa na asilimia 10 ya fedha zote zilizopokelewa.

Mchechu ameeleza kuwa,ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa mazingira ya biashara pamoja na utekelezaji wa mageuzi mbalimbali ya kiutendaji, kiutawala na kiusimamizi yaliyoongeza ufanisi, tija na faida katika mashirika ya umma.

Mbali na hayo, Rais Dkt.Samia amesema, ameridhishwa na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa mwaka 2025 wakati wa hafla kama hiyo, akibainisha kuwa ongezeko la gawio ni ishara kuwa taasisi za umma zina uwezo wa kuboresha utendaji wake na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

“Ninafuraha kuona maelekezo niliyoyatoa mwaka jana yamefanyiwa kazi. Kuongezeka kwa gawio la Serikali kwa asilimia 30 ni uthibitisho kwamba mashirika ya umma yanaweza kutoa huduma bora kwa wananchi na wakati huo huo kuwa nguzo muhimu ya ujenzi wa uchumi wa nchi,”amesema.

Amesisitiza kuwa,Siku ya Gawio isiwe tukio la kusherehekea mafanikio ya kifedha pekee, bali iwe fursa ya kutathmini utendaji wa taasisi hizo na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kuongeza tija na ufanisi.

Rais Dkt.Samia pia amewapongeza viongozi na watendaji wa mashirika yote yaliyofanikiwa kutoa gawio kwa Serikali, akisema mchango wao ni sehemu muhimu ya jitihada za kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu akizungumza kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Gawio na Michango kutoka kwa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Gawio na Michango kutoka kwa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.

Hata hivyo, ameonya kuwa Serikali haitavumilia uzembe, matumizi mabaya ya rasilimali za umma wala utendaji usio na tija, akisisitiza kuwa hatua stahiki zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwamisha maendeleo ya taasisi za umma.

“Pongezi hizi zisiwe sababu ya kuridhika au kubweteka.Serikali itaendelea kusimamia uwajibikaji, ufanisi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma ili kuhakikisha taasisi zote zinatoa mchango unaostahili katika maendeleo ya Taifa,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here