Rais wa Singapore Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam kufanya ziara ya Kitaifa nchini Tanzania kuanzia Juni 8 hadi 10,2026

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam,anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 08 hadi 10 Juni 2026, kwa mwaliko wa mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma leo Juni 5,2026 na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mheshimiwa Rais Shanmugaratnam anaweka historia ya kuwa Rais wa kwanza wa Singapore kutembelea nchini tangu kuanzishwa ushirikiano wa kidiplomasia mwaka 1980, ambapo ziara hii inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Singapore.

Vilevile, ziara hiyo inaonesha dhamira ya pamoja ya nchi hizi mbili katika kuendeleza ushirikiano wa kimkakati unaolenga kukuza maendeleo ya kiuchumi, biashara, uwekezaji, ubunifu na maendeleo endelevu.

Wakati wa ziara hiyo, viongozi hao wawili wanatarajiwa kuwa na mazungumzo rasmi yatakayolenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na biashara na uwekezaji, maendeleo ya bandari na usafirishaji,uchumi wa kidijitali, utalii, elimu, mafunzo ya ujuzi, pamoja na maendeleo ya miundombinu na teknolojia.

Aidha, ziara hiyo itatoa fursa ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Singapore, nchi ambazo zimeendelea kushirikiana kwa misingi ya kuheshimiana, usawa, na maslahi ya
pamoja tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia mnamo tarehe 12 Desemba 1980.

Mhe. Rais Tharman ambaye ataambatana na Mwenza wake, Mama Jane Ittogi Shanmugaratnam, Mawaziri, Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Singapore na ujumbe wa Wafanyabiashara wa Singapore, atapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabiti Kombo (Mb.), katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 08 Juni 2026.

Tarehe 09 Juni 2026, Mhe. Rais Tharman Shanmugaratnam atapokelewa rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Baada ya mapokezi hayo, viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha yakifuatiwa na mazungumzo rasmi kuhusu
uhusiano kati ya Tanzania na Singapore.

Mazungumzo hayo yatafuatiwa na taarifa ya pamoja itakayotolewa na Viongozi hao kwa Waandishi wa Habari kuhusu masuala mbalimbali waliyokubaliana na baadaye Rais Tharman Shanmugaratnam atashiriki Dhifa ya Kitaifa itakayoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Siku hiyo hiyo, Mhe. Rais Shanmugaratnam na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia Dkt. Suluhu Hassan watashiriki Jukwaa la Biashara na Uwekezaji litakalowashirikisha Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Tanzania na Singapore.

Aidha, tarehe 10 Juni 2026, Mhe. Rais Shanmugaratnam atakwenda Zanzibar kuendelea na ziara yake ambako pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi na baadaye jioni Mhe. Rais Shanmugaratnam na ujumbe wake wataondoka kurejea Singapore.

Ziara hii ya kihistoria inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili na kuchochea fursa zaidi za uwekezaji, biashara, na ushirikiano wa watu kwa watu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here