NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Guinea ya Ikweta imejiuzulu rasmi baada ya kushindwa kufikia malengo ya utendaji iliyokuwa imewekewa, hatua iliyotangazwa na Makamu wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mangue ambaye pia ni mtoto wa Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu Manuel Osa Nsue Nsua aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa niaba ya mawaziri wote wa serikali kufuatia tathmini iliyoonesha kuwa serikali hiyo ilifanikiwa kutekeleza chini ya asilimia 10 ya malengo yake ya maendeleo na utendaji.
Obiang amesema,hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia kanuni ya uwajibikaji katika utumishi wa umma, akisisitiza kuwa viongozi wa serikali wanapaswa kupimwa kwa matokeo ya kazi zao.
“Uwajibikaji katika usimamizi wa umma lazima uambatane na matokeo yanayoonekana. Kiwango cha utekelezaji kilichofikiwa ni kidogo mno ukilinganisha na matarajio na ahadi zilizotolewa,”amenukuliwa Makamu wa Rais na vyombo vya habari kutoka Malabo, Guinea ya Ikweta
Ingawa hakufafanua kwa kina malengo yaliyoshindikana kutekelezwa, taarifa iliyotolewa na Chama Tawala cha Democratic Party of Equatorial Guinea (PDGE) imeeleza kuwa,Rais Obiang hajaridhishwa na utendaji wa serikali hiyo kutokana na kushamiri kwa vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kushindwa kusukuma mbele miradi muhimu ya maendeleo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Obiang amebaini kuwa,baadhi ya viongozi walitumia rasilimali za serikali kwa manufaa binafsi badala ya kuendeleza maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Aidha, serikali iliyomaliza muda wake ilikosolewa kwa kushindwa kutekeleza sera za kuimarisha na kufanya uchumi wa nchi kuwa wa sekta mbalimbali badala ya kutegemea sekta moja.
Rais amesisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta ya kilimo ili kupunguza utegemezi mkubwa wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi wakati baadhi yake zinaweza kuzalishwa ndani ya Guinea ya Ikweta.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaeleza kuwa,changamoto ya utegemezi wa mafuta imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo endelevu ya taifa hilo, huku juhudi za kuimarisha sekta mbadala zikisonga kwa kasi ndogo.
Guinea ya Ikweta ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi barani Afrika. Sekta hiyo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya serikali pamoja na mauzo ya nje ya nchi.
Hata hivyo, licha ya utajiri huo wa rasilimali za mafuta, sehemu kubwa ya wananchi wa taifa hilo lenye wakazi takribani milioni 1.8 imeendelea kukabiliwa na umaskini.
Ripoti mbalimbali zimekuwa zikionesha kuwa, faida za utajiri wa mafuta hazijasambazwa kwa usawa miongoni mwa wananchi.
Katika miaka ya hivi karibuni, uchumi wa nchi hiyo umekuwa ukidorora kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa mafuta pamoja na kushuka kwa mahitaji ya bidhaa hiyo katika soko la kimataifa.
Hali hiyo imeongeza shinikizo kwa serikali kutafuta vyanzo vipya vya ukuaji wa uchumi na ajira.
Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1979 na kutambulika kama kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani, anatarajiwa kuunda serikali mpya katika siku zijazo.
Serikali iliyovunjwa ilikuwa imeteuliwa mwaka 2024 chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Manuel Osa Nsue Nsua.
Kujiuzulu kwa pamoja kwa mawaziri wote kunafungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini humo huku wananchi na wadau wa maendeleo wakisubiri kuona iwapo serikali mpya itaweza kukabiliana na changamoto zilizotajwa, hususan rushwa, usimamizi wa rasilimali za umma na mageuzi ya uchumi.
Hatua hiyo inaonekana kuwa ishara ya shinikizo kubwa ndani ya utawala wa Guinea ya Ikweta la kutaka kuona matokeo ya haraka katika utekelezaji wa sera za maendeleo, wakati taifa hilo likikabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili.
