DODOMA-Serikali imeendelea kutumia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), kama nyenzo muhimu ya kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma kwa wananchi na kuvutia uwekezaji nchini.
Hayo yameelezwa na Mchumi Mwandamizi wa Kitengo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Wizara ya Fedha, Bi. Josephina Melkiol wakati akizungumza na wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Alisema katika kufanikisha hilo Serikali imefanya maboresho ya Sera, Sheria na Kanuni za PPP ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo hadi kufikia Juni 2026, jumla ya mikataba tisa (9) ya PPP imesainiwa katika sekta mbalimbali za maendeleo.
“Miradi iliyosainiwa ni pamoja na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) Awamu ya Kwanza na ya Pili wenye jumla ya mikataba minne, Mradi wa Ukaguzi wa Lazima wa Vyombo vya Moto, Mradi wa Ujenzi na Uendeshaji wa Jengo la Biashara Kariakoo, Mradi wa Ukarabati na Uendeshaji wa Reli ya TAZARA pamoja na miradi ya uboreshaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kupitia Kampuni za DP World na ADAN,” alibainisha Bi. Josephina.
Alieleza kuwa,Serikali ilianzisha utekelezaji wa Programu ya PPP kupitia Sera ya Taifa ya PPP ya mwaka 2009, iliyolenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, alisema Sheria ya PPP ya mwaka 2010 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2011 ziliweka msingi wa mfumo wa kisheria na kitaasisi wa kusimamia miradi hiyo, huku marekebisho yaliyofanyika mwaka 2014, 2018 na 2023 yakilenga kuongeza ufanisi katika maandalizi ya miradi na mchakato wa kupata wabia.
Bi. Josephina alisema,Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya mfumo wa PPP ili kuongeza uwekezaji katika sekta za kimkakati, kuboresha miundombinu na kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi.
Aliongeza kuwa,ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unaendelea kuwa chachu muhimu ya maendeleo kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali, teknolojia na utaalamu unaohitajika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa.
Tags
Chinangali Park Dodoma
Habari
PPP Tanzania
Wiki ya Utumishi wa Umma Tanzania
Wizara ya Fedha Tanzania





