NA DIRAMAKINI
WAKATI Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI ikiendelea kusisitiza ubora wa elimu nchini, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wameibua wasiwasi kuhusu kile wanachodai kuwa ni tabia ya baadhi ya shule kuendelea kuwaita wanafunzi darasani wakati wa likizo rasmi, jambo ambalo wanasema linanyima wanafunzi haki yao ya kupumzika na kuwa karibu na familia zao.
Malalamiko hayo yanakuja wakati wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wakiwa katika likizo ya mwezi Juni, kipindi ambacho kimekusudiwa kuwapa muda wa kupumzika baada ya miezi kadhaa ya masomo.Hata hivyo, baadhi ya wazazi na walezi wanadai kuwa watoto wao wamekuwa wakitakiwa kufika shuleni kuanzia asubuhi hadi jioni kwa ajili ya masomo ya ziada, huku wengine wakihudhuria hata siku za Jumamosi na Jumapili.
Kwa mujibu wa wakazi hao, hali hiyo imeanza kuibua maswali kuhusu utekelezaji wa ratiba rasmi za elimu na kiwango cha usimamizi wa mamlaka husika katika kuhakikisha shule zote zinafuata miongozo iliyowekwa.
Mkazi wa Kinondoni, Juma Mwakalinga, anasema likizo ni sehemu muhimu ya mchakato wa kujifunza na haiwezi kutenganishwa na maendeleo ya mwanafunzi.
“Mtoto anahitaji muda wa kupumzika baada ya kipindi kirefu cha masomo.Likizo si adhabu wala si muda wa kuendelea na ratiba zilezile za shule. Serikali inapaswa kufuatilia shule zinazopuuzia ratiba rasmi,”amesema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Asha Mrope, mkazi wa Temeke ambaye anasema,baadhi ya wazazi wamejikuta wakibeba gharama zisizotarajiwa kutokana na watoto wao kuendelea kwenda shuleni hata wakati wa likizo.
“Wazazi wengi hupanga matumizi yao wakijua mtoto atakuwa nyumbani wakati wa likizo. Lakini shule zinapoendelea kuwaita wanafunzi, mzazi analazimika kuendelea kugharamia usafiri, chakula na mahitaji mengine,”amesema.
Umuhimu wa Likizo
Wataalamu wa elimu wanaeleza kuwa,likizo ni sehemu ya msingi katika mfumo wa elimu duniani. Mbali na kupunguza uchovu wa kimwili na kiakili, likizo huwapa wanafunzi nafasi ya kushiriki shughuli za kijamii, kujifunza stadi za maisha na kuimarisha uhusiano wao na familia.
Aidha, tafiti mbalimbali zimekuwa zikionesha kuwa mwanafunzi anayepata muda wa kutosha wa kupumzika huwa na uwezo mkubwa wa kurejea darasani akiwa na ari mpya ya kujifunza na uwezo mzuri wa kuzingatia masomo.
Kutokuwepo kwa muda wa mapumziko kunaweza kuongeza msongo wa mawazo, uchovu na kupunguza hamasa ya kujifunza, hali ambayo inaweza kuathiri matokeo ya muda mrefu ya kielimu.
Pia,baadhi ya wachambuzi wa elimu wanaona kuwa sababu mojawapo inayochangia shule kuendesha masomo wakati wa likizo ni ushindani mkubwa wa kitaaluma na hamu ya kupata matokeo bora katika mitihani ya taifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, shule nyingi zimekuwa zikipimwa kwa kiwango kikubwa kupitia matokeo ya wanafunzi wake, jambo ambalo limeongeza presha kwa walimu na viongozi wa shule kutafuta muda zaidi wa kufundisha.
Hata hivyo, wadau wa elimu wanaonya kuwa mafanikio ya kitaaluma hayapaswi kupatikana kwa gharama ya ustawi wa mwanafunzi.
“Ubora wa elimu haupimwi kwa idadi ya saa ambazo mwanafunzi anatumia darasani pekee, bali pia kwa mazingira anayojifunzia na ustawi wake wa jumla,”amesema Hassan Khamis, mkazi wa Ubungo.
Kutokana na hali hiyo, wakazi wa Dar es Salaam wameiomba Serikali kupitia Waziri wa Elimu kutoa tamko rasmi na kuchukua hatua kali dhidi ya shule zitakazobainika kukiuka ratiba za likizo zilizowekwa na mamlaka za elimu.
Wanasema hatua hizo zinapaswa kujumuisha ukaguzi wa mara kwa mara, utoaji wa maelekezo ya wazi kwa shule zote pamoja na kuwawajibisha watakaobainika kwenda kinyume na taratibu.
Kwa mujibu wa wadau hao, utekelezaji madhubuti wa sheria na kanuni za elimu utasaidia kulinda haki za wanafunzi na kuhakikisha ratiba rasmi zinazotolewa na Serikali zinaheshimiwa na kila taasisi ya elimu nchini.
Aidha,kadiri mjadala kuhusu masomo ya likizo unavyoendelea, jambo moja linaonekana wazi; elimu bora inahitaji uwiano kati ya kujifunza na kupumzika.
Wakati shule zikijitahidi kuinua kiwango cha ufaulu, ni muhimu pia kutambua kuwa ustawi wa mwanafunzi ni msingi wa mafanikio ya kweli ya kielimu.
Hivyo basi, Serikali, wazazi, walimu na wadau wengine wa elimu wanapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa haki za wanafunzi zinalindwa na na likizo zilizowekwa rasmi zinatimiza lengo lake la kuwajengea wanafunzi afya bora ya akili, mwili na mazingira mazuri ya kujifunzia.