Simba SC yapanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara

NA DIRAMAKINI

KLABU Simba (Simba SC) ya jijini Dar es Salaam imeendelea kuonesha dhamira yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu huu.
Ni baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliochezwa leo Juni 17,2026 kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Ushindi huo muhimu umeiwezesha Simba SC kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 64, hatua inayoongeza kasi ya mbio zake za kusaka taji la ligi huku msimu ukielekea ukingoni.

Bao pekee la mchezo huo limefungwa na mshambuliaji Elie Mpanzu ambaye ameendelea kuthibitisha ubora wake katika safu ya ushambuliaji ya Simba.
Mfungaji huyo sasa ameandika rekodi ya kufunga katika mechi tatu mfululizo za ligi, baada ya hapo awali kuzitikisa nyavu za Dodoma Jiji na Pamba Jiji.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulizikutanisha timu mbili zenye malengo tofauti, Simba ikisaka alama tatu muhimu katika mbio za ubingwa huku Mbeya City ikipigania kujiweka katika mazingira salama dhidi ya hatari ya kushuka daraja.

Aidha,baada ya bao hilo la mapema, pande zote mbili zilijaribu kutengeneza nafasi za kufunga kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza na ya kujenga, lakini uimara wa safu za ulinzi pamoja na umakini wa walinda mlango ulihakikisha kuwa matokeo hayabadiliki hadi dakika ya mwisho ya mchezo.

Mwamuzi Ahmada Simba kutoka Kagera alipuliza filimbi ya mwisho huku Simba ikiondoka na alama zote tatu muhimu zilizowapa furaha mashabiki wake na kuimarisha nafasi yao katika kilele cha msimamo.
Ushindi huo pia ni wa saba mfululizo kwa Simba katika Ligi Kuu NBC Tanzania Bara tangu ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Young Africans SC mnamo Mei 3, 2026. Mfululizo huo wa matokeo mazuri unaonyesha uthabiti wa kikosi hicho katika kipindi muhimu cha mwisho wa msimu.

Kwa upande wa Mbeya City, kipigo hicho kimeongeza presha katika harakati zake za kujinusuru kushuka daraja. Timu hiyo sasa inakabiliwa na mechi tatu za mwisho ambazo zinaweza kuamua mustakabali wake katika ligi kuu.

Mbeya City itahitaji kupata matokeo chanya katika michezo dhidi ya Dodoma Jiji, Pamba Jiji na TRA United ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kubaki kwenye ligi msimu ujao.

Baada ya kumaliza jukumu la ligi, Simba sasa itaelekeza nguvu zake katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambapo itakutana na Coastal Union katika mchezo wa nusu fainali utakaochezwa Juni 20,2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kwa upande wa Mbeya City, macho na matumaini yao yataelekezwa kwenye mchezo ujao wa ligi dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Juni 24, 2026 katika dimba la CCM Kirumba huku wakihitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kusalia katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Matokeo ya leo yameonesha wazi kuwa mbio za ubingwa bado zinaendelea kuwa ngumu na zenye ushindani mkubwa, huku Simba ikituma ujumbe mzito kwa wapinzani wake kwamba bado ipo imara katika harakati za kutwaa taji la msimu wa 2025/2026.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here