NA DIRAMAKINI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imemkamata aliyekuwa Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Amani Mlaya ambaye alikuwa akitafutwa na vyombo vya dola baada ya kutoroka mahakamani kinyume na masharti ya dhamana yake katika shauri la jinai namba 000011512 la mwaka 2024.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema,mtuhumiwa huyo alikamatwa katika eneo la Mangaka Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, alipokuwa amejificha baada ya kutoroka wakati wa hatua za mwisho za shauri lililokuwa linamkabili mahakamani.
Ngailo amesema,uchunguzi na msako uliofanywa na mamlaka husika uliwezesha kubaini mahali alikokuwa akijificha na hatimaye kukamatwa ili kuanza kutumikia adhabu iliyotolewa na mahakama.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, kabla ya kutoroka, mahakama ilikuwa imemkuta na hatia katika makosa manne kati ya sita aliyokuwa akikabiliwa nayo na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikwepa kutekeleza hukumu hiyo baada ya kutoroka siku iliyokuwa imepangwa kwa ajili ya kusomwa kwa hukumu ya shauri lake.
Ngailo ameeleza kuwa,baada ya kutoroka kwa mshtakiwa huyo, mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwake na kuagiza kwamba aanze kutumikia kifungo chake mara tu atakapopatikana.
Amesema,kukamatwa kwa Mlaya ni matokeo ya ushirikiano kati ya vyombo vya dola na wananchi katika kuhakikisha kuwa watuhumiwa na wahalifu wanaokwepa mkono wa sheria wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Amani Mlaya alikuwa akikabiliwa na jumla ya makosa sita, yakiwemo manne ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2022.
Pia alikuwa akikabiliwa na makosa mengine chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, Marejeo ya mwaka 2022.
TAKUKURU imesisitiza kuwa,itaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya dola,wananchi katika kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayekwepa utekelezaji wa sheria na kwamba hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, udanganyifu na makosa mengine ya jinai yanayohujumu uchumi wa taifa.
Aidha,kukamatwa kwa mshtakiwa huyo kunatajwa kuwa sehemu ya jitihada zinazoendelea za kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha hukumu zinazotolewa na mahakama zinatekelezwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
