■ Asisitiza Ushirikiano na Ubunifu katika Utoaji Haki
NA HALIMA MNETE,
Mahakama-Dodoma
MTENDAJI Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Anthony Jingu, amesema atahakikisha anaendeleza mafanikio yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania sambamba na kuleta ubunifu mpya utakaozidi kuimarisha utoaji wa haki nchini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu akitoa neno wakati wa kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu huyo na kumuaga Mtendaji Mkuu Mstaafu, Prof. Elisante Ole Gabriel kilichofanyika tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo jana tarehe 24 Juni, 2026 katika kikao maalum cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu huyo mpya wa Mahakama na kumuaga kwa heshima Mtendaji Mkuu mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel baada ya kuhitimisha utumishi wake wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Jingu amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani kubwa aliyomuwekea kwa kumteua kushika nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, akisema uteuzi huo ni heshima kubwa kwake na dhamana nzito inayohitaji kujituma, uadilifu na unyenyekevu wa hali ya juu.
Amesema amepokea dhamana hiyo kwa heshima kubwa akitambua uzito wa majukumu yanayoambatana na nafasi hiyo, huku akiahidi kuyatekeleza kwa bidii na kwa moyo wa kuitumikia nchi.
Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama waliohudhuria katika kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu huyo na kumuaga Mtendaji Mkuu Mstaafu, Prof. Elisante Ole Gabriel kilichofanyika tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.“Ninapokea dhamana hii kwa heshima kubwa na unyenyekevu. Ninafahamu uzito wa jukumu hili na matarajio makubwa yaliyopo. Kwangu, utekelezaji wa nafasi hii si wajibu wa kawaida bali ni ibada na huduma kwa taifa,” alisema Dkt. Jingu.
Aidha, alisema mwelekeo wa uongozi wa Serikali chini ya Rais Samia umejikita katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, usalama na ustawi wa wananchi, huku taasisi za umma zikiendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na uwajibikaji. Alisisitiza kuwa Mahakama kama mhimili muhimu wa dola ina nafasi ya kipekee katika kufanikisha maelekezo hayo kupitia utoaji wa haki wenye usawa, weledi na uadilifu.
Dkt. Jingu amesema atayapokea na kuyafanyia kazi maelekezo ya Rais kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha Mahakama inaendelea kuwa taasisi imara inayojenga imani kwa wananchi.
“Maelekezo ya Mhe. Rais ni dira muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu. Tutahakikisha Mahakama inaendelea kutimiza wajibu wake kwa viwango vinavyotarajiwa na wananchi wa Tanzania,” ameongeza.
Pamoja na hayo, Dkt. Jingu amempongeza Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel, kwa uongozi wake wa mafanikio na mchango mkubwa alioutoa katika kuimarisha utendaji wa Mahakama kwa kipindi chote cha utumishi wake.
Amesema Prof. Gabriel ameacha alama kubwa ndani ya Mahakama kupitia uongozi wake uliosaidia kusukuma mbele mageuzi mbalimbali ya kimfumo na kiutendaji yaliyoongeza ufanisi katika utoaji haki.
Dkt. Jingu pia amempongeza Prof. Gabriel kwa kustaafu akiwa na afya njema, akieleza kuwa hali hiyo ni ushahidi wa maisha yenye nidhamu pamoja na umuhimu wa kuwa na familia bora inayotoa upendo, utulivu na msaada wa karibu.
“Tumeshuhudia Prof. Gabriel akihitimisha utumishi wake akiwa mwenye afya njema, jambo ambalo ni la kujivunia. Hii inaonesha umuhimu wa kuwa na familia bora na mazingira mazuri ya maisha yanayompa mtu utulivu na nguvu ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” ameeleza.
Aidha, alisema nasaha na hekima zilizotolewa na Prof. Gabriel wakati wa makabidhiano hazitapuuzwa, badala yake zitafanyiwa kazi kwa vitendo ili kuendeleza misingi mizuri iliyoachwa.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu wakati wa kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu huyo mpya wa Mahakama na kumuaga kwa heshima Mtendaji Mkuu mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel kilichofanyika tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akimkaribisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu wakati wa kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu huyo mpya wa Mahakama na kumuaga kwa heshima Mtendaji Mkuu mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel kilichofanyika tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma).
Amesisitiza kuwa mafanikio ya taasisi hayawezi kupatikana kwa juhudi za mtu mmoja pekee bali yanahitaji ushirikiano wa viongozi na watumishi wote.
“Ujenzi wa Taasisi imara si kazi ya mtu mmoja. Tunahitaji kushirikiana, kusaidiana na kujengana ili tuweze kufikia malengo yetu ya pamoja,” amesema.
Dkt. Jingu amewahimiza Viongozi na watumishi wa Mahakama kuendelea kumpa ushirikiano pamoja na kumwelekeza pale inapohitajika, akisema bado yupo katika mchakato wa kujifunza na yuko tayari kupokea maarifa mapya kutoka kwa wote wenye uzoefu.
“Tutaendeleza yote mazuri tuliyoyakuta, lakini pia tutaleta mawazo mapya, ubunifu mpya na mifumo mipya itakayozidi kuimarisha utendaji wa Mahakama,” amesema.
Aliongeza kuwa, Mahakama haipaswi kujikita katika tafsiri ya sheria pekee, bali pia katika kuzingatia utu, maadili na ubinadamu katika utoaji wa huduma kwa wananchi, ili haki itolewe kwa namna inayolinda hadhi ya kila mmoja.




