TAKUKURU yawafikisha mahakamani watumishi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika kwa tuhuma za uhujumu uchumi na ubadhirifu wa shilingi milioni 126.82

NA DIRAMAKINI

WATUMISHI wawili wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika (LTBWB) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma tarehe 3 Juni,2026 wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali za uhujumu uchumi, ubadhirifu wa mali ya umma na kughushi nyaraka, zinazohusisha kiasi cha Shilingi milioni 126.82.
Shauri hilo la jinai lenye namba ECC.12182/2026 lilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Mhe. Anna Kuhungu.

Kwa mujibu wa upande wa Jamhuri, washtakiwa hao ni Matei Francis Mkanta, ambaye ni mhadrolijia, na Madua Mrisho Rusumbunya, dereva wa taasisi hiyo. 

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa ya Matumizi ya Nyaraka Kumdanganya Mwajiri, Ufujaji na Ubadhilifu, Kusaidia kutendeka kwa Kosa na Kughushi; Kinyume na Kifungu cha 22, 28(1) na 30 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 R. E 2022.

Vifungu hivyo vikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 RE 2022 pamoja na Kifungu cha 333, 335(a), 335(b)(i)(ii) cha Kanuni za Adhabu Sura 16 Marejeo ya mwaka 2022.

Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka 2022, washtakiwa hao walidaiwa kuandaa na kutumia hati zenye taarifa za uongo zilizoidhinisha malipo ya jumla ya Shilingi 126,820,000, fedha zinazodaiwa kuwa mali ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika.

Inadaiwa kuwa nyaraka hizo zilikuwa na maelezo ya uongo kuhusu malipo yaliyolenga watumishi hewa waliodaiwa kushiriki shughuli za utambuzi na ukaguzi wa vyanzo vya maji katika Wilaya za Kigoma, Kasulu na Uvinza pamoja na Manispaa ya Kigoma-Ujiji.

Washtakiwa wote wawili walipofikishwa mahakamani walikana mashtaka yote 72 yanayowakabili. Hata hivyo, walishindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama na hivyo kupelekwa mahabusu hadi hatua nyingine za kisheria zitakapochukuliwa.

Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Juni 18, 2026, litakaporejea kwa hatua zaidi za usikilizwaji.

Kesi hiyo inaendeshwa na mawakili wa upande wa mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Augustino Lohay na Bw. James Nyarobi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here