Waziri Ridhiwani Kikwete awataka Wanafunzi wa Sheria kujijengea nidhamu,uzalendo na ubunifu kukabiliana na ushindani wa ajira duniani

NA DIRAMAKINI

WANAFUNZI wa sheria nchini wametakiwa kujenga misingi imara ya taaluma zao kwa kuzingatia nidhamu, uzalendo,maadili na ubunifu ili kuwawezesha kushindana kwa ufanisi katika soko la ajira la kimataifa ambalo linaendelea kuwa na ushindani mkubwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kazi duniani.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kazi na Taaluma ya Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika Juni 5,2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kikwete amesema kuwa,taaluma ya sheria ni miongoni mwa nyanja muhimu zinazohitaji wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma,maadili ya kazi na uzalendo ili waweze kutoa mchango chanya katika maendeleo ya taifa na kuhimili ushindani wa kimataifa.

Alieleza kuwa,katika zama za sasa,mafanikio ya kitaaluma hayaamuliwi tu na ufaulu wa darasani,bali pia na uwezo wa mhitimu kutumia maarifa yake katika mazingira halisi ya kazi,kushindana na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali na kuzingatia maadili ya taaluma yake.
"Ni muhimu kwa wanafunzi wa sheria kutambua kuwa dunia ya ajira imebadilika kwa kiwango kikubwa. Leo,ushindani haupo ndani ya mipaka ya nchi pekee,bali ni wa kimataifa. Hivyo, nidhamu, uzalendo,uadilifu na umahiri wa kitaaluma ni nguzo muhimu zitakazowasaidia kufanikiwa,”amesema.

Aidha, Waziri Kikwete aliwataka wanafunzi hao kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na kasi ya mabadiliko yanayotokea katika sekta ya sheria na mifumo ya utoaji haki duniani.

Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa taaluma ya sheria ina nafasi kubwa katika kusimamia haki, kulinda maslahi ya wananchi na kuimarisha utawala bora, hivyo ni wajibu wa wanafunzi na wataalamu wa sheria kuhakikisha wanazingatia viwango vya juu vya maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Sambamba na hilo, Waziri huyo alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza mageuzi makubwa yenye lengo la kuimarisha sekta ya sheria na utoaji wa haki nchini.
Alifafanua kuwa,mageuzi hayo yanahusisha maboresho ya mfumo wa haki, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kisheria, uwekezaji katika miundombinu ya mahakama na taasisi nyingine za haki pamoja na kuimarisha mifumo mbadala ya utatuzi wa migogoro.

Kwa mujibu wa Waziri Kikwete, hatua hizo zimekusudiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki, kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuweka mazingira bora zaidi kwa wataalamu wa sheria kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.

Aliongeza kuwa,serikali imeendelea kuwekeza katika mifumo inayowawezesha wanasheria, waendesha mashtaka, mahakimu, majaji na wadau wengine wa sekta ya haki kufanya kazi katika mazingira yanayokidhi mahitaji ya wakati na maendeleo ya teknolojia.
“Kuimarishwa kwa sekta ya sheria na haki ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Taifa haliwezi kufikia maendeleo endelevu bila kuwa na mfumo imara wa utoaji haki unaojenga imani kwa wananchi na wawekezaji,”amesema.

Waziri huyo alibainisha kuwa,mchango wa wataalamu wa sheria ni muhimu katika kulinda maslahi ya taifa, kuimarisha utawala wa sheria, kusimamia haki na kuchochea mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here