Waziri wa Fedha awataka walipakodi kuendelea kulipa kodi kwa hiari,asisitiza mapato ndiyo msingi wa miradi mikubwa ya maendeleo

DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amewataka walipakodi nchini kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, kwa wakati na kwa ukamilifu,kwa kuwa mapato ya ndani ndiyo yanayowezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa Hafla ya Mbio na Matembezi ya Shukrani kwa Mlipakodi, iliyofanyika katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam kuelekea Tuzo za Rais kwa Mlipakodi Bora pamoja na Maadhimisho ya Miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mhe. Balozi Omar amesema kuwa, Serikali inaitegemea TRA kukusanya takribani Shilingi trilioni 36 katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mapato ya ndani yanayotarajiwa kufikia shilingi trilioni 46, ambayo yatachangia zaidi ya asilimia 34 ya bajeti ya Serikali.

Amesema kuwa,mafanikio ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yanaonesha ushirikiano mzuri kati ya Serikali na walipakodi, huku akieleza kuwa mwezi uliopita TRA ilivuka lengo la ukusanyaji kwa asilimia tatu na kueleza matumaini ya kufikia malengo ya mwaka mzima ifikapo Juni 30.

"Kila mwaka wa fedha tunaanza upya, Tunapoingia Julai tunaanza safari mpya yenye malengo makubwa zaidi. Tunawatakia wafanyabiashara na wawekezaji mafanikio katika shughuli zao za kiuchumi, lakini mafanikio hayo yaende sambamba na kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa hiari, kwa wakati na kwa ukamilifu,"amesema Mhe. Balozi Khamis.
Aidha, Mhe.Balozi Omar amebainisha kuwa, maendeleo makubwa yanayoendelea kushuhudiwa nchini, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), uboreshaji wa Reli ya TAZARA pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), yametekelezwa kwa kiasi kikubwa kupitia mapato yanayotokana na kodi zinazolipwa na wananchi na wafanyabiashara.

Amesema,Reli ya Kisasa ya SGR imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri kwa kubeba maelfu ya abiria kwa safari moja, jambo linalopunguza msongamano wa usafiri wa barabarani na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi nchini.

Mhe. Balozi Omar amewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, akieleza kuwa afya bora huongeza tija mahali pa kazi, hupunguza gharama za matibabu na kuongeza uzalishaji wa kiuchumi, jambo ambalo pia huchangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali.

“Nawataka watumishi wa TRA, walipakodi pamoja na washauri wa kodi, muendelee kushiriki mazoezi ya viungo, kwa kuwa mwili wenye afya huongeza uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kutoa huduma bora kwa wananchi,”amesema Mhe. Balozi Omar.
Vilevile, Mhe. Balozi Omar amesisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano nchini, akibainisha kuwa mazingira hayo ndiyo msingi wa ukuaji wa biashara, uwekezaji na ukusanyaji wa mapato.

"Bila amani na utulivu shughuli za kiuchumi haziwezi kufanyika, ni wajibu wetu sote kuendelea kulinda amani ya nchi yetu ili wananchi waendelee kufanya kazi, kuzalisha, kupata kipato na kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa,"amesema Mhe.Balozi Omar.

Aidha,Mhe.Balozi Omar ameipongeza TRA kwa kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake na kuwapongeza walipakodi wote kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa kupitia ulipaji wa kodi, huku akitoa wito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, walipakodi na wadau wa kodi ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),CPA Yusuph Juma Mwenda amesema,ushirikiano mzuri kati ya TRA na walipakodi umeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya ukusanyaji wa mapato nchini.

CPA Mwenda amesema kuwa, mafanikio hayo yanatokana na kujengeka kwa uaminifu na ushirikiano kati ya TRA na walipakodi, jambo linalochangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

“TRA imeendelea kutekeleza maboresho makubwa ya kiutendaji, kimfumo na kiteknolojia yenye lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa walipakodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, huku matumizi ya mifumo ya kidijitali yamepunguza urasimu, kuongeza uwazi na uwajibikaji, pamoja na kurahisisha walipakodi kupata huduma kwa haraka na kwa urahisi,"amesema CPA Mwenda.
Amesisitiza kuwa,TRA itaendelea kuwekeza katika ubunifu, matumizi ya teknolojia na utoaji wa elimu kwa walipakodi ili kuimarisha mazingira rafiki ya biashara, kuongeza wigo wa walipakodi na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here