Waziri wa Fedha,Mheshimiwa Balozi Omar ashiriki Bonanza la Bunge kuendeleza hamasa za AFCON 2027

DODOMA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wameungana na viongozi mbalimbali wa Serikali, Waheshimiwa Wabunge na wadau wa maendeleo kushiriki Bonanza la Bunge lililoandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya CRDB, likiwa na kaulimbiu isemayo “Pamoja AFCON 2027, Tanzania Tupo Tayari.”
Bonanza hilo lililoongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo (Mb), lilianza kwa matembezi ya pamoja kutoka Viwanja vya Bunge kuelekea Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ambapo Matembezi hayo yalilenga kuhamasisha afya njema, mshikamano na ushiriki wa wananchi katika maandalizi ya michuano mikubwa ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda.
Katika bonanza hilo, washiriki walipata fursa ya kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mbio fupi, pete, bao na kuvuta kamba.

Michezo hiyo iliwakutanisha viongozi, watumishi wa umma na wadau wengine katika mazingira yaliyojaa ushindani wa kirafiki, burudani na kujenga mahusiano mema.

Ushiriki wa Waziri wa Fedha na Naibu wake katika bonanza hilo unaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya AFCON 2027, pamoja na kutambua mchango wa michezo katika kuimarisha afya, umoja na maendeleo ya kijamii.
Aidha, bonanza hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuendeleza hamasa ya kitaifa kuelekea AFCON 2027, huku likiwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kujadili na kuunga mkono jitihada zinazoendelea kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kupokea na kuandaa mashindano hayo kwa viwango vya kimataifa.

Kupitia kaulimbiu ya “Pamoja AFCON 2027, Tanzania Tupo Tayari,” washiriki walituma ujumbe wa mshikamano na uzalendo, wakisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kuwa sehemu ya safari ya maandalizi ya mashindano hayo makubwa ambayo yanatarajiwa kuleta fursa za kiuchumi, kijamii na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here