■Kikombe kimoja cha Kahawa kinauzwa shilingi 10,000 huku Mkulima akipata Shilingi 150 tu,nani anachukua Shilingi 9,850 zilizobaki?
NA SAFARI FUNGO
JUNI 4,2026 ndani ya Gasper Hotel and Conference Centre iliyopo Ihumwa jijini Dodoma nilipata bahati kutoa mhadhara juu ya uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko ya Kahawa.
Katika mada yangu, nilitumia mfano mmoja unaoonesha kwa uwazi changamoto na fursa iliyopo katika sekta ya kahawa duniani.
Leo hii, katika masoko mengi yaliyoendelea mathalani kwenye mgahawa uliopo London, kikombe kimoja cha kahawa kinaweza kuuzwa kwa wastani wa Shilingi 10,000 za Tanzania au zaidi.
Hata hivyo, uchambuzi wa mnyororo wa thamani wa kahawa unaonesha kuwa kati ya kiasi hicho, sehemu inayotokana na kahawa ghafi inayozalishwa na mkulima ni takribani Shilingi 150 tu.Kwa maneno mengine, kati ya kila Shilingi 10,000 anayolipa mlaji kwa kikombe kimoja cha kahawa, ni karibu asilimia 1.5 pekee ndiyo inayohusishwa na kahawa inayozalishwa shambani.
Ukiendelea kuchambua mnyororo huo wa thamani, unaona kuwa sehemu nyingine huenda kwa usindikaji, usafirishaji, biashara za kati ama ukaangaji wa kahawa.
Hata hivyo, sehemu kubwa zaidi ya bei ya mwisho huenda kwenye shughuli za kuongeza thamani kama mishahara ya wafanyakazi, kodi, upangishaji wa maeneo ya biashara, maziwa na viambato vingine, vifaa vya kutumika, huduma kwa wateja, masoko na faida za biashara zinazouza kahawa hiyo kwa mlaji wa mwisho.
Ni muhimu kuelewa kuwa hali hii haimaanishi kwamba mkulima anadhulumiwa moja kwa moja.
Ukweli ni kwamba mteja anayelipa Shilingi 10,000 hanunui kahawa ghafi pekee; analipia pia huduma, uzoefu wa matumizi, mazingira ya biashara, ubora wa maandalizi ya kahawa, chapa, urahisi wa upatikanaji na thamani nyingine nyingi zinazoongezwa njiani.
Hata hivyo, takwimu hizi zinatoa somo muhimu sana kwa nchi zinazozalisha kahawa kama Tanzania.
Sehemu kubwa ya thamani ya kiuchumi haizalishwi shambani bali katika hatua za baada ya uzalishaji.
Ndiyo maana, licha ya kuwa wazalishaji wakubwa wa kahawa, nchi nyingi zinazozalisha kahawa bado hupata sehemu ndogo ya mapato yanayotokana na biashara ya kahawa duniani.
Badala ya kuendelea kuuza malighafi pekee, tunapaswa kujenga uwezo wa kushiriki zaidi katika hatua za usindikaji, ukaangani wa kahawa, ufungashaji, chapa, usambazaji na hata biashara za mwisho zinazomfikia mlaji.
Hapo ndipo thamani kubwa zaidi na fursa kubwa za ajira, uwekezaji na mapato zinapopatikana.
Kwa Tanzania, ujumbe wangu ulikuwa wa wazi kwamba hatuwezi kubadilisha maisha ya wakulima kwa kuzalisha kahawa nyingi zaidi pekee.
Tunahitaji pia kuongeza thamani ya kahawa yetu na kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa Thamani duniani.
Kadiri tunavyoongeza ushiriki wetu katika uchakataji, ubunifu wa bidhaa na masoko ya walaji wa mwisho, ndivyo sehemu kubwa zaidi ya zile Shilingi 10,000 za kikombe cha kahawa itakavyobaki mikononi mwa Wakulima wa kitanzania.






