NA DIRAMAKINI
HUDUMA za Mahakama ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma zimeanza kutolewa rasmi, hatua inayolenga kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na umbali wa kufuata mashauri katika maeneo mengine.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 29, 2026 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Joachim C. Tiganga, huduma hizo zilianza rasmi Julai 24, 2026 katika jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chamwino lililopo Kata ya Chamwino Ikulu, karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chamwino.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuzingatiwa kwa masharti ya Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 ya mwaka 1984, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, pamoja na Tangazo la Serikali Na. 215/2026 lililofuta mamlaka ya Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kusikiliza mashauri yanayotokea Wilaya ya Chamwino.