NA DIRAMAKINI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara imetangaza rasmi kuanza kwa zoezi la kupokea maombi ya ukodishaji wa mashamba ya halmashauri kwa msimu wa kilimo wa 2026/2027, ikiwataka wananchi, vikundi na taasisi kujitokeza kuomba mashamba hayo kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Teresia A. Irai mashamba yanayopatikana kwa ukodishaji yapo katika maeneo ya Gawal, lenye ukubwa wa ekari 586 na Bassotu Plantation, lenye ukubwa wa ekari 8,254.Tangazo hilo linaeleza kuwa,mashamba hayo yana udongo wenye rutuba unaofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali, yakiwemo ngano, shayiri, mahindi, mbaazi, alizeti, karanga, maharage, dengu, vitunguu pamoja na mazao mengine ya msimu.
Kwa mujibu wa halmashauri, kiwango cha ada ya ukodishaji kwa msimu wa 2026/2027 kitakuwa shilingi 250,000 kwa ekari katika shamba la Gawal, huku shamba la Bassotu Plantation likitozwa kati ya Shilingi 100,000, 150,000 na 200,000 kwa ekari, kutegemeana na aina ya udongo wa eneo analochagua mwombaji.
Aidha, Halmashauri imetangaza kuwa ekari 123 zitatolewa bila malipo kwa waombaji watakaokidhi vigezo vilivyowekwa.
Kwa mujibu wa masharti ya ukodishaji, waombaji watatakiwa kulipa ada ya maombi isiyorejeshwa ya Shilingi 50,000 kwa maombi ya shamba lisilozidi ekari 50 na Shilingi 100,000 kwa maombi ya shamba lenye zaidi ya ekari 50, baada ya kupata namba ya malipo (Control Number) kutoka Ofisi ya Mweka Hazina wa Halmashauri.
Fomu za maombi zinapatikana katika Ofisi ya Afisa Usimamizi wa Ununuzi wa Halmashauri kuanzia Julai 1 hadi Julai 15, 2026, na zinapaswa kujazwa kikamilifu pamoja na kuthibitishwa na Mtendaji wa Kijiji au Kata husika kabla ya kurejeshwa.
Halmashauri imeeleza kuwa waombaji watakaofanikiwa watasaini mikataba ya ukodishaji kwa msimu mmoja wa kilimo, utakaoanza Novemba 1, 2026 hadi Oktoba 31, 2027.
Waombaji hao pia watapaswa kulipa ada ya ukodishaji ndani ya siku 30 tangu watangaziwe idadi ya ekari walizopangiwa. Endapo mwombaji hatalipa ndani ya muda uliowekwa bila sababu za msingi, eneo hilo litapewa mwombaji mwingine.
Aidha, wakodishaji wataoneshwa mipaka ya mashamba yao rasmi na timu ya Halmashauri kabla ya kuanza shughuli za kilimo, na hawataruhusiwa kulima eneo lolote kabla ya kukabidhiwa rasmi ili kuepusha migogoro ya ardhi.
Mashamba hayo yatatumika kwa shughuli za kilimo cha mazao ya chakula na biashara pekee, huku Halmashauri ikisisitiza kuwa haitawajibika kwa hasara yoyote itakayojitokeza wakati wa uzalishaji, kwani gharama zote za uendeshaji wa shughuli za kilimo zitabebwa na mkodishaji.
Vilevile, wakodishaji wametakiwa kutunza mazingira kwa kutoharibu vyanzo vya maji au maeneo ya mazingira yaliyopo ndani ya mashamba hayo.
Mwisho wa kupokea maombi ni Jumatatu, Julai 20, 2026 saa 9:30 alasiri, ambapo fomu zote zinapaswa kuwa zimewasilishwa katika Ofisi ya Manunuzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.
Halmashauri imewahimiza wananchi, vikundi na taasisi zenye uwezo wa kuwekeza katika kilimo kuchangamkia fursa hiyo kwa kufuata masharti yote yaliyotolewa ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo wilayani Hanang’.
