DODOMA-Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kuwa kitovu cha utoaji wa taarifa za utafiti wa madini nchini Tanzania baada ya kupokea ugeni kutoka nchini Uganda uliokuja kujifunza masuala mbalimbali kuhusu taasisi hiyo na sekta ya madini kwa ujumla.
Ujumbe huo umepokelewa Julai 27, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Prof. Abdulkarim Mruma uliopo katika ofisi za GST, Dodoma, ukiongozwa na Bi. Agnes Alaba, Kamishna wa Madini kutoka Idara ya Madini nchini Uganda.
Kwa upande wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), mazungumzo hayo yameongozwa na Mtendaji Mkuu, Mhandisi Ally Samaje, Pamoja na Viongozi wa Idara na Sehemu zake.
Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa GST, Mhandisi Ally Samaje, amesema taasisi imeendelea kuwa kitovu cha utoaji wa taarifa za utafiti wa madini kwa wazawa na wageni.
Pia amebainisha kuwa GST imeendelea kujiimarisha kifedha na kitaalamu kupitia majukumu yake, ambayo mengine yamejikita kibiashara ikiwemo utoaji wa huduma za kimaabara, ushauri elekezi na mauzo ya machapisho mbalimbali.
Amebainisha kuwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Wizara ya Madini na taasisi zilizo chini yake umeendelea kuchangia maendeleo makubwa katika sekta ya madini, ambayo ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi na kuchangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aliongeza kuwa hatua hiyo imesaidia Serikali kuridhia kutenga asilimia 10 ya makusanyo yanayotokana na sekta ya madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za madini nchini, jambo ambalo ni hatua kubwa kwa taasisi.
Mhandisi Samaje amewahakikishia Idara ya Jiolojia ya Uganda, iliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ya Uganda, kuwa GST iko tayari kutoa ushirikiano wa kujifunza namna ambavyo taasisi hiyo imepitia michakato mbalimbali hadi kuwa taasisi kamili.
Ameeleza kuwa ilianzishwa mwaka 1925 na Serikali ya kikoloni, baadaye ikawa Idara chini ya Wizara ya Nishati na Madini, mwaka 2005 ikawa Wakala, na hatimaye kuwa Taasisi kupitia mabadiliko ya Sheria ya Madini.
Sambamba na hayo, Meneja wa Jiolojia wa GST, Bw. Solomon Maswi, ameueleza ugeni huo majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na taasisi, muundo wake, machapisho mbalimbali yaliyofanywa tangu kuanzishwa kwake, huduma zinazotolewa, pamoja na hatua za utafiti na maeneo ya nchi yaliyofikiwa katika upimaji wa kijiolojia, ambapo hadi sasa ni asilimia 97 ya maeneo yamefikiwa na asilimia 3 iliyobaki inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2030.
Amefafanua kuwa taasisi pia ina maabara za kisasa zenye vifaa vya kisasa, wataalamu wenye ujuzi na uzoefu wa hali ya juu pamoja na ithibati ya kimataifa kwa ajili ya kufanya huduma za upimaji na uchenjuaji.
Aidha, amesema kwa sasa GST ina ofisi Dodoma na Geita inayohudumia wateja wa Kanda ya Ziwa, huku ujenzi wa ofisi nyingine ukiendelea mkoani Mbeya ambayo itahudumia wateja wa mikoa ya Kanda ya Kusini.
Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe huo, Bi. Agnes Alaba, amefurahishwa na mafanikio ya GST katika tafiti zake pamoja na mfumo wa ushauri elekezi unaoiwezesha taasisi hiyo kuwa bunifu na kujinufaisha kiuchumi na kitaaluma kupitia shughuli za ushauri elekezi.
Amesema hatua hiyo imewawezesha wataalamu wa GST kumudu ushindani katika soko la huduma za utafiti wa rasilimali.
Ujumbe wa Idara ya Jiolojia kutoka nchini Uganda umeanza ziara ya siku nne nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza namna ambavyo GST imefanikiwa kubadilisha mifumo yake ya kiutendaji na kimuundo hadi kuwa taasisi kamili inayotekeleza majukumu yake kwa uhuru.
Tags
Habari
Kimataifa
Sekta ya Madini Tanzania
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)










