MARA-Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama, Mrakibu wa Polisi (SP) Jeremiah Zitta, amewahimiza wananchi kutumia kila fursa wanayoipata kuwasaidia wengine, akisema kufanya hivyo ni njia ya kuonyesha upendo na kuwafariji wenye uhitaji.
SP Zitta ameyasema hayo Julai 29, 2026, wakati alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, ambapo alikabidhi mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa kama sehemu ya kuonyesha upendo na mshikamano na jamii.
Pia, SP Zitta aliambatana na Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Butiama, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ponsian Kalinjuma, pamoja na Maafisa na askari wa vyeo mbalimbali ambapo walipokelewa na Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Asha Mayunga.
Akizungumza katika zoezi hilo, ASP Kalinjuma alisema Jeshi la Polisi linathamini maisha ya kila mwananchi na linaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda usalama wa watu na mali zao.
Alibainisha kuwa kutembelea makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo wagonjwa, ni sehemu ya utamaduni wa Jeshi la Polisi unaolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya wananchi na jeshi hilo.
Aidha, ASP Kalinjuma alitoa elimu kwa wagonjwa na ndugu zao kuhusu umuhimu wa kushiriki katika ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi, hatua ambayo alisema itasaidia kuzuia na kutokomeza uhalifu katika jamii.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama, Dkt. Asha Mayunga, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada wa mahitaji mbalimbali, maneno ya faraja na elimu waliyoitoa kwa wagonjwa.
Ameeleza kuwa hatua hiyo imeleta faraja kwa wagonjwa na kuomba shughuli kama hizo ziendelee ili kuimarisha mshikamano kati ya taasisi za umma na wananchi.
Baadhi ya wagonjwa waliopokea msaada huo pia wameishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwajali na kuwapa faraja pamoja na elimu ya ulinzi na usalama.


