Tanzania yachukua rasmi uenyekiti wa Kundi la Afrika katika Kamati ya Urithi wa Dunia

BUSAN-Tanzania imechukua rasmi Uenyekiti wa Kundi la Afrika katika Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO kwa kipindi cha miaka miwili ijayo baada ya kuhitimishwa kwa mafanikio Kikao cha 48 cha Kamati hiyo kilichofanyika Busan, Jamhuri ya Korea.
Sambamba na jukumu hilo, Tanzania pia itahudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Urithi wa Dunia, Mjumbe wa Bureau ya Kamati hiyo na Mjumbe wa Bureau ya Mkutano Mkuu wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972.

Akizungumza wakati wa kuhitimishwa kwa mkutano, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Mhe. Saidi Othman Yakubu, alisema Tanzania inathamini imani iliyopewa na nchi za Afrika na imejipanga kutekeleza wajibu huo kwa weledi, mshikamano na kujituma ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Senegal.

Aidha, Tanzania imewashukuru kwa dhati Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Korea kwa maandalizi bora na ukarimu mkubwa walioonesha wakati wote wa mkutano, pamoja na Sekretarieti ya Kituo cha Urithi wa Dunia cha UNESCO, Mkurugenzi wake na watumishi wote kwa kuratibu kikao hicho kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Katika kikao hicho, Tanzania ilitoa mchango mkubwa katika mijadala mbalimbali ya Kamati, iliandaa kwa mafanikio kongamano maalum kuhusu Hifadhi ya Ngorongoro, na iliendelea kuzungumza kwa niaba ya Kundi la Afrika katika masuala mbalimbali ya urithi wa dunia, ikisisitiza mshikamano wa bara na ushirikiano wa kimataifa katika kulinda urithi wa dunia kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here