NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua Semina Elekezi ya Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Mawasiliano Serikalini katika Ikulu ya Tunguu,Zanzibar.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Semina Elekezi kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Mawasiliano Serikalini, tarehe 28 Julai, 2026, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar.
Semina hiyo ya siku mbili ambayo imefunguliwa Julai 28,2026 imewakutanisha, kwa mara ya kwanza, viongozi waandamizi wa Serikali kutoka pande zote mbili za Muungano, kwa lengo la kujenga uelewa na msimamo wa pamoja kuhusu mawasiliano ya Serikali na umma.Akizungumza wakati wa ufunguzi, Rais Dkt. Samia amesema,mawasiliano ya Serikali yanahitaji uratibu, weledi na mwelekeo wa kimkakati ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na kulinda maslahi ya Taifa.
"Mawasiliano ni sehemu ya uongozi na nyenzo ya kimkakati ya kulinda maslahi ya Taifa," amesema Rais Dkt. Samia.
Ameeza kuwa,mawasiliano yanapotumika vizuri hujenga ushirikishwaji na imani ya wananchi kwa Serikali, huku taarifa sahihi zikiwawezesha kuelewa na kushiriki katika mipango ya maendeleo."Taarifa za Serikali zinapaswa kutolewa kwa wakati, kwa lugha inayoeleweka na kwa takwimu zilizothibitishwa,"amesema.
Rais Dkt. Samia amesema,Serikali zote mbili zimepata mafanikio katika sekta za elimu, afya, miundombinu, nishati na maeneo mengine ya maendeleo, ambayo yanapaswa kuelezwa kwa wananchi kwa ufasaha.
Kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema Serikali zote mbili zimeanza kutekeleza mageuzi makubwa ya uchumi na huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja.Amesema,takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira 2050 inategemea ushiriki wa sekta binafsi, hivyo mafanikio yake yanahitaji mawasiliano na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta hiyo.
Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt.Moses Mpogole Kusiluka amesema,semina hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia ya kuwajengea viongozi uwezo katika mawasiliano ya Serikali na umma.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Mosses M. Kusiluka akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Semina Elekezi kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Mawasiliano Serikalini, tarehe 28 Julai, 2026, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Prof. Palamagamba A. Kabudi akitoa mada inayohusu Muungano na Mawasiliano; Msingi, Muundo na Umuhimu wake wakati wa ufunguzi wa Semina Elekezi kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Mawasiliano Serikalini, tarehe 28 Julai, 2026, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar.Amesema,mafunzo hayo yatahusu utoaji wa taarifa kwa ufasaha na kwa wakati, pamoja na matumizi sahihi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.








