Rais Dkt.Samia athibitisha nia ya maridhiano kuelekea mchakato wa maboresho ya Katiba

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema,Serikali itaendeleza maridhiano ya kisiasa kuelekea hatua za maboresho ya Katiba kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,Bakari S.Machumu ambapo Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Julai 30,2026 alipokutana na viongozi wa vyama 18 vya siasa nchini, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalihusu maridhiano, mageuzi ya kisiasa, uchumi, huduma za jamii, ajira, uwekezaji na ulinzi wa amani ya nchi.

Akirejea hatua ya mchakato wa maridhiano visiwani Zanzibar, Rais Dkt.Samia aliwaeleza viongozi hao hatua zilizofikiwa za maandalizi ya mchakato wa maridhiano kuelekea hatua zinazofuata za mapitio ya Katiba.
Amesisitiza kuwa,hatua zote za mchakato huo zitafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu zilizowekwa, kwa maslahi mapana ya Taifa, na kwamba Serikali itaendelea kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa mazungumzo katika kipindi cha angalau mara tatu kwa kila mwaka.

Mkutano huo, uliowaleta pamoja wenyeviti, makamu wenyeviti, makatibu wakuu na viongozi wa jumuiya za vyama vya siasa nchini, ni wa pili wa aina hiyo kuitishwa na Rais Dkt. Samia tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mkutano wa awali ulifanyika Machi 31, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha wagombea wa nafasi ya Rais na wagombea wenza kutoka vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumzia taswira ya uchumi wa nchi, Rais Dkt. Samia alisema uchumi wa nchi umeendelea kukua kwa asilimia sita katika mwaka uliopita, huku ukuaji wa asilimia 6.3 ukitarajiwa mwaka huu.
Amesema, Serikali imeweka msisitizo katika kukamilisha miradi ya maendeleo iliyokwishaanza kutekelezwa, pamoja na kuendeleza uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli, barabara, bandari na miundombinu mingine.

Katika uwekezaji, Rais Dkt. Samia amesema, maboresho yaliyofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia biashara ya ndani na kikanda, na kubainisha kuwa Serikali inaendelea na upanuzi wa shughuli katika bandari za Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amevitaka vyama vya siasa nchini kulinda amani, uhuru na maslahi ya nchi, akisisitiza kuwa ulinzi wa Tanzania ni wajibu wa pamoja baina ya Serikali, vyama vya siasa na wananchi wote.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chama Cha AAFP Said Soud Said mara baada ya mkutano na Viongozi wa Vyama vya Siasa nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Julai, 2026.

Katika hatua nyingine, viongozi hao waliwasilisha maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wananchi katika nyanja za siasa, maendeleo ya jamii na uchumi. Serikali iliahidi kuendelea kuyapokea na kuyafanyia kazi mapendekezo hayo kupitia majukwaa stahiki ya majadiliano na mifumo rasmi ya maamuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here