Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii-Waziri wa Fedha

NA BENNY MWAIPAJA
Tanga

SERIKALI imeahidi kutoa shilingi Milioni 750 ili kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyosalia katika Kituo kipya cha Afya Kange, kilichopo katika kata ya Maweni, jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi katika kata hiyo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiwa amembeba mtoto Eunice Allen, aliyefika na mzazi wake kupata huduma ya mama na mtoto, katika Kituo cha Afya Kange, kilichoko Kata ya Maweni Jijini Tanga, wakati alipopita kuwasalimia wananchi waliofika kupata huduma baada ya kuweka jiwe la Msingi katika mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho ambacho mpaka sasa ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi milioni 694 na kikikamilika kujengwa kitakuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi 40,000. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Fedha).

Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Tanga ambapo alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Kituo cha Afya Maweni,mradi wa mabweni katika Shule Kongwe ya Sekondari Usagara na Mradi wa Ukarabati wa Shule Kongwe ya Msingi Funguni Wilaya ya Pangani.

“Baada ya kuwasilishwa kwa maombi ya fedha za kukamilisha ujenzi wa Kituo hiki na uongozi, nimenong’ona na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga na Mkuu wa Wilaya na baada ya majadiliano yao wamenieleza kuwa zinahitajika shilingi milioni 750, ili majengo yote yakamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi, nitawasiliana na mkoa, Halmashauri ya Jiji na Wizara ya Fedha ili kiasi hicho kipatikane na kukamilisha ujenzi,"amesema Mhe. Balozi Omar.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akihutubia katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika Kituo kipya cha Afya Kange, kilichopo katika kata Maweni, jijini Tanga, ambacho kitahudumia wananchi wapatao 40,740 wa kata hiyo, ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za uzazi na matibabu.
Amewataka wakazi wa mkoa huo kufuata maelekezo ya wataalam wa afya kupunguza maradhi kwa kutunza mazingira, kuchemsha maji ya kunywa, kusafisha maeneo ya makazi ili kuua vimelea vinavyosababisha marafhi ikiwemo kipindupindu na kwa wale watakao ugua basi wakitumie kikamilifu Kituo hicho cha Afya Kange.

Mhe. Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa wananchi kukitunza kituo hicho cha afya ili kiweze kuwafaa kwa muda mrefu

Aidha,Mhe.Balozi Omar amebainisha kuwa,kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026, Serikali imejitahidi kuwekeza kwa kiasi kikubwa cha fedha katika Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Kwa mwaka huu wa fedha uliopita, Mkoa wa Tanga ulipangiwa kutumia Shilingi bilioni 528.1, na Serikali imewasilisha kiasi cha shilingi bilioni 487.5. Sawa na ufanisi wa asilimia 92 ya fedha zote zilizopangwa kutolewa,"amesisitiza Mhe. Balozi Omar.

Kwa upande wake,Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba aliishukuru Serikali, kwa kuipatia Wilaya yake kiasi cha shilingi bilioni bilioni 350 zilizoelekezwa kuekekeza miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za wananchi katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.

Kwa upande wao Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Abdulrahman Shillow, Mganga Mkuu wa Jiji (DMO), Dkt.Stephen Mwandambo walieleza kuwa kituo hicho cha Maweni ni mkombozi kwa wananchi wapatao 40,740 wa kata hiyo, ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za uzazi na matibabu.
Aidha, alieleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga shilingi milioni 75 kwa ajili ya mwaka wa fedha ujao ili kukamilisha ujenzi wa baadhi ya majengo yaliyobaki, ikiwemo kuchomea taka, ukamilishaji wa jengo la upasuaji, na wodi ya wazazi, ili kuimarisha huduma katika kituo hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here