NA LWAGA MWAMBANDE
SHILINGI ya Tanzania ni zaidi ya chombo cha kubadilishia thamani ya bidhaa na huduma, ni alama ya mamlaka ya Taifa, utambulisho wa kiuchumi na sehemu muhimu ya mfumo wa fedha unaowezesha shughuli za kila siku za wananchi.
Katika kipindi ambacho uchumi wa dunia unakabiliwa na mabadiliko mbalimbali, ni muhimu kwa Watanzania wote kuendelea kuthamini na kuheshimu sarafu yao ya Taifa kwa kuitumia kwa uadilifu na kuilinda dhidi ya vitendo vinavyoweza kudhoofisha thamani yake.
Heshima kwa Shilingi ya Tanzania inaanza na matumizi sahihi ya fedha hiyo, ikiwemo kuzuia vitendo vya kughushi,uharibifu wa noti na sarafu, pamoja na tabia ya kupuuza matumizi ya fedha ya ndani katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Fedha ya Taifa ina nafasi kubwa katika kujenga uchumi imara kwa sababu ndiyo msingi wa biashara, uwekezaji, malipo ya huduma na mzunguko wa shughuli za kiuchumi ndani ya nchi.
Kadiri wananchi wanavyoendelea kuiamini na kuitumia kwa uwajibikaji, ndivyo inavyozidi kuwa na nafasi ya kuchangia ukuaji wa uchumi.
Aidha, taasisi za fedha na wadau mbalimbali wana wajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi fedha, kutambua alama za usalama zilizowekwa kwenye noti na kutoa taarifa pale wanapobaini vitendo vya ukiukwaji vinavyohusiana na sarafu ya Taifa.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, kuheshimu Shilingi ya Tanzania ni sehemu ya uzalendo na kujenga mazingira bora ya kiuchumi. Kila mwananchi ana nafasi ya kulinda hadhi ya fedha ya Taifa kwa kuitumia kwa uangalifu, kuithamini na kuhakikisha inaendelea kuwa nyenzo muhimu katika maendeleo ya nchi. Endelea;
1. Shilingi ya Tanzania, ni vema iheshimiwe,
Jinsi tunavyotumia, kwa uzuri itumiwe,
Sifa kuiharibia, ni vema kulaaniwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
2. Pesa kwa Uchumi wetu, ukue tuinuliwe,
Biashara ada zetu, huko kote itumiwe,
Shilingi maisha yetu, hufanya tuhudumiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
3. Tumetangaziwa sana, Shilingi iheshimiwe,
Vile tunavyoiona, vema sana itumiwe,
Kurusharusha Hapana, hufanya ichafuliwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
4. Huwa tunazo sherehe, na watuwashangiliwe,
Cha kwetu kimuhemuhe, watu pesa wapatiwe,
Wachungaji na Mashehe, na wao tusaidiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
5. Unazionesha pesa, wengine wakuelewe,
Tayarisha chombo hasa, humo ndimo zitupiwe,
Hili la bure darasa, ni vema litambuliwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
6. Vema watu kuwatunza, chombo na kiandaliwe,
TanTrade napongeza, na Kibati waenziwe,
Kuweka chombo liweza, watu pesa wapatiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
7. Shilingi heshima yetu, vema sana ienziwe,
Hata matumizi yetu, na isidharauliwe,
Iwe ni wajibu wetu, isifike tukemewe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
8. Kwa wote washereheshaji, hili budi muelewe,
Mdomo wenu mtaji, wateja na waambiwe,
Mtakuwa wakosaji, kesho tusilaumiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
9. Onesha unazo pesa, kitaka ushangiliwe,
Unapoziweka pesa, vema sana paelewe,
Kutupatupa ni kosa, singoje ushitakiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
10. Kwenye cherekochereko, ninyi nyote muelewe,
Acheni hivi vituko, ifike mtambuliwe,
Mara ufike mkoko, na nyie mnyakuliwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
11. Viongozi wa jamii, hata dini muelewe,
Eleza watu watii, kesho wasiadhibiwe,
Bila shuruti utii, vema sana uenziwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
12. Haya mambo ya Katoro, ni vema yalaaniwe,
Hiyo ni kubwa kasoro, wenye huku muelewe,
Ni makosa tena kero, kokote yasirudiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
