TANGA-Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati mkoani Tanga ili kuufungua mkoa huo kiuchumi na kurejesha hadhi yake ya kuwa kitovu cha viwanda nchini.
Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Khamis Mussa Omar (Mb), alipokutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo upanuzi wa Bandari ya Tanga, uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Tanga, ujenzi wa barabara pamoja na reli ya kisasa (SGR), hatua ambazo zitaongeza fursa za ajira, biashara na uwekezaji.
Alisema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 429 katika upanuzi wa Bandari ya Tanga, ambapo uwezo wa Bandari hiyo umeongezeka kwa kiwango kikubwa na tayari imeanza kuhudumia meli kubwa zinazobeba shehena na makontena mengi zaidi.
"Wananchi wa Tanga wanaanza kuona matokeo ya uwekezaji huu. Bandari imepanuliwa kwa kiwango kikubwa na uwezo wake umeongezeka maradufu. Hii ni hatua muhimu katika kuifungua Tanga kiuchumi,"alisema Mhe. Balozi Omar
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha mradi wa reli ya Tanga–Arusha–Musoma unatekelezwa kwa mujibu wa mipango, huku ikiendelea kuboresha mtandao wa barabara unaounganisha Tanga na mikoa mingine pamoja na nchi jirani ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.
Katika sekta ya afya, alisema Serikali itafuatilia upatikanaji wa fedha za kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tanga na kushughulikia changamoto zilizobainishwa wakati wa ziara hiyo.
Aidha, alisema Serikali itafanya tathmini ya kina kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa barabara ya Tanga–Pangani na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Mhe. Balozi Omar alisema maoni na changamoto zilizokusanywa kutoka kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Tanga zitawasilishwa Serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha ahadi zote zinazotolewa kwa wananchi zinatekelezwa kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC), Mohammed Salim, alimshukuru Waziri wa Fedha kwa kutembelea Mkoa wa Tanga, alisema ziara hiyo imeongeza hamasa ya kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aliahidi kuwa Chama kitaendelea kuhamasisha wananchi kutumia fursa za kiuchumi na kushirikiana na Serikali katika kusukuma mbele maendeleo ya mkoa huo, huku akisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara, reli, bandari na miundombinu mingine muhimu kwa ukuaji wa uchumi.










