Waziri wa Fedha atoa maagizo kwa Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na watumishi wa Hazina Ndogo nchini

TANGA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameiagiza Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na watumishi wa Hazina Ndogo nchini kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora, zenye heshima, utu na weledi kwa wastaafu wanaolipwa pensheni na Hazina.
Agizo hilo alilitoa alipokuwa akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Hazina Ndogo mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo, ambapo alisisitiza kuwa wastaafu ni kundi muhimu linalostahili kuthaminiwa kutokana na mchango mkubwa walioutoa katika ujenzi wa Taifa walipokuwa watumishi wa umma.

Mhe. Balozi Omar alisema huduma bora kwa wastaafu huongeza ustawi wao na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali, huku akiwataka watumishi kuwahudumia kwa uvumilivu, kuwapa maelekezo sahihi na kuwasaidia kukamilisha taratibu za uhakiki bila usumbufu usio wa lazima.
Aliwataka pia watumishi kuendelea kutoa elimu kwa wastaafu kuhusu kujihadhari na matapeli wanaojifanya mawakala wa huduma za pensheni, akisisitiza kuwa huduma za pensheni na taratibu za uhakiki hazihitaji mstaafu kutoa fedha kwa mtu binafsi.

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, ambaye pia ni Msimamizi wa Ofisi za Hazina Ndogo nchini, alimshukuru Waziri wa Fedha kwa kutembelea Ofisi ya Hazina Ndogo Tanga na kuzungumza na watumishi, akisema hatua hiyo imewatia moyo na kuwapa hamasa ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

CPA Mkude alimshukuru Mhe. Balozi Omar kwa kuwawezesha watumishi kupata ujuzi kupitia mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi, hatua ambayo itaongeza uwezo wao wa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aliahidi kuwa watumishi wa Hazina Ndogo Tanga wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na unyenyekevu mkubwa ili kuhakikisha wananchi, hususan wastaafu wanaolipwa pensheni kupitia Hazina, wanapata huduma stahiki kwa wakati na kwa heshima inayostahili, ikiwa ni kutambua mchango wao mkubwa walioutoa katika kulitumikia Taifa.
Alizungumzia kuhusu huduma zinazotolewa na Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Mkude alisema kuwa Hazina Ndogo ni sehemu muhimu ya mfumo wa Serikali katika usimamizi wa fedha za umma nchini.

Ofisi hizo zimeanzishwa mahsusi kwa lengo la kusogeza huduma za Hazina karibu na taasisi za Serikali zinazotekeleza bajeti katika ngazi za mikoa, na hivyo kuongeza ufanisi, uwajibikaji, uwazi na nidhamu ya fedha katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Alisema kuwa kwa sasa, Ofisi za Hazina Ndogo zipo katika mikoa yote 25 ya Tanzania Bara, na zote zinafanya kazi chini ya Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali.

Kupitia Ofisi hizi, Serikali imeweza kuimarisha usimamizi wa mapato, matumizi, malipo ya Serikali, usuluhishi wa hesabu za kibenki, pamoja na usimamizi wa pensheni na mafao mengine yanayolipwa kupitia Hazina.
Katika ziara hiyo katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Tanga, Mhe. Balozi Omar aliambatana na baadhi ya Wakuu wa Idara wakiwemo Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Dkt. Remidius Ruhinduka, Kamishna Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, Bw. Bashiru Taratibu na pia Mkuu wa Hazina Ndogo Tanga Bi. Akwilina Kirita na Msimamizi wa Mali za Serikali Mkoa huo Bw. Salum Matimbwa pamoja na wafanyakazi wote wa Hazina ndogo na Msimamizi wa Mali za Serikali Mkoa wa Tanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here