TANGA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ametembelea Kampuni ya kutengeneza samani ya Burhan Furniture iliyopo jijini Tanga na kuwataka wamiliki wa kampuni hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kukuza biashara yao, kuifikisha katika masoko ya kimataifa na kuchangia kuongeza fursa za ajira pamoja na mapato ya Serikali.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Balozi Omar alisema Serikali inaendelea kuthamini mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa, hivyo akawasisitiza wawekezaji kuendelea kuimarisha uzalishaji, kuongeza ubora wa bidhaa na kutumia fursa zilizopo ili kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, aliwataka viongozi na wamiliki wa Burhan Furniture kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa uaminifu, akieleza kuwa mapato ya kodi ndiyo msingi wa Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii.
"Niwapongeze kwa uwekezaji wenu na mchango wenu katika kutoa ajira kwa Watanzania. Endeleeni kufanya kazi kwa bidii, kuboresha uzalishaji na kulipa kodi kwa uaminifu ili muendelee kuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa letu," alisema Mhe. Balozi Omar
Kwa upande wao, viongozi wa Burhan Furniture walimshukuru Waziri wa Fedha kwa kutembelea Kampuni yao na kueleza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza uwekezaji, kuzingatia sheria za kodi na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Katika ziara hiyo, Mhe. Balozi Omar aliambatana na mwenyeji wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, pamoja na viongozi wengine.





