Uthabiti wa uchumi ni matokeo ya usimamizi thabiti wa Benki Kuu-Gavana Tutuba

DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amesema,uthabiti wa uchumi wa Tanzania unaodhihirishwa na mfumuko wa bei unaobaki katika kiwango cha takriban asilimia 4 ni matokeo ya usimamizi madhubuti wa sera za fedha na mifumo ya kifedha inayotekelezwa na Benki Kuu.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la BoT katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Saba Saba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Julai 10,2026, Gavana Tutuba amesema,maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza kuhusu kazi za Benki Kuu na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Gavana Tutuba amebainisha kuwa,uamuzi wa hivi karibuni wa kuweka kiwango cha riba ya Benki Kuu kuwa 6.25% unalenga kuhakikisha kunakuwa na ukwasi wa kutosha katika sekta ya benki, kukuza utoaji wa mikopo na kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
Amesema,Tanzania imeendelea kuwa na uchumi imara unaovutia wawekezaji licha ya changamoto za kiuchumi duniani, huku akieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na usimamizi wa kitaalamu wa sera za fedha, mifumo salama ya malipo na uwekezaji endelevu katika kuwajengea uwezo wataalamu wa Benki Kuu.

Katika ziara hiyo, Gavana Tutuba amepata pia maelezo kuhusu mfumo wa Sema na BoT, ambao umeongeza ufanisi katika upokeaji na utatuzi wa malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha.

Ameagiza mfumo huo uendelee kuboreshwa ili uweze kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo wasioweza kutumia mifumo ya kidijitali kwa urahisi.
Gavana Tutuba amesema,Benki Kuu inajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, ikiwemo kuimarika kwa uthabiti wa sekta ya fedha, kuongezeka kwa ujumuishaji wa kifedha, kuimarika kwa mifumo ya malipo na kuongezeka kwa taasisi za fedha zinazotoa huduma kwa wananchi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here