NA VERONICA MWAFISI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua changamoto ya ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na ndio maana kati ya vipaumbele vya Serikali vilivyopo, ajira ni mojawapo.
Mhe. Kikwete amesema hayo leo tarehe 10 Julai, 2026 wakati akizungumza na Viongozi, Watumishi wa Umma na Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kabla ya kukagua na kuzindua Shule ya Msingi Ilolangula Mlimani katika Wilaya hiyo.
“Serikali inafahamu changamoto ya ajira hususan katika sekta ya Elimu na Afya na ndio maana Rais wetu mpendwa amekuwa akitoa vibali vya ajira, huku akifafanua kuwa mwaka huu wa fedha 2026/27 kibali cha ajira kwa watumishi 45,000 kimetolewa ambapo Sekta ya Elimu itafaidika pia,” amesisitiza Mhe. Kikwete.
Ameongeza kuwa haya yote yanafanyika kwasababu Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwajali wananchi wake hasa katika kupata huduma bora huku akiwasisitiza wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii kwani elimu ni muhimu kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
“Suala la elimu linasisitizwa sana hata katika vitabu vyote vitakatifu vya dini, hivyo wanafunzi hamna budi kusoma kwa bidii ili kuwa na ufahamu wa mambo mengi kwa maendeleo ya taifa letu,” ameongeza.
Katika hatua nyingine Mhe. Kikwete amuelekeza Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga Ofisi ya TAKUKURU wilayani Uyui.
Amesema Ofisi ya TAKUKURU ina umuhimu wake katika kuzuia na kupambana na rushwa katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Wilaya hiyo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Mohamed Mtulyakwaku aliwasilisha changamoto kwa Mhe. Waziri Kikwete kuwa Wilaya yake inakabiliwa na uhaba wa Watumishi hasa katika Sekta ya Elimu na Afya, hivyo aliiomba Serikali kuwapatia watumishi hao ili waweze kuwadumia wananchi kikamilifu.
“Tunatambua kuwa Serikali imekuwa ikituletea watumishi wapya lakini bado tuna uhitaji, hivyo tunaomba mtufikirie katika hili,” aliongeza Mkuu wa Wilaya huyo.
Aidha, alizungumzia suala la kutokuwepo kwa Ofisi ya TAKUKURU katika Wilaya hiyo kwani wamekuwa wakisafiri mpaka Tabora mjini kufuata huduma hiyo pale wanapoihitaji.
Waziri Ridhiwani Kikwete anahitimisha leo ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.







