NA GODFREY NNKO
SERIKALI imesema,sheria zinapaswa kutumika kama nyenzo ya maendeleo ya taifa badala ya kuwa mfumo wa udhibiti pekee, huku ikisisitiza kuwa ubora wa sheria hupimwa kwa matokeo yake katika kuboresha maisha ya wananchi, kuvutia uwekezaji, kuimarisha utawala bora na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 10,2026 wakati wa uzinduzi wa kitabu kipya cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia (Mama Samia Doctrine of Law): Utekelezaji Wake katika Mageuzi ya Kiuchumi na Kijamii, uliofanyika katika Ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).Kitabu hicho kimezinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, na kimeelezwa kuwa ni andiko la kwanza la kina linalochambua kitaaluma nafasi ya sheria katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Abdulla amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza Johari kwa kuja na wazo la kuandikwa kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia ambacho kimeeleza kwa kina kuhusu nafasi ya sheria katika maendeleo ya taifa.
Amesema, kitabu hicho ambacho kimeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili wa Serikali kimebeba maudhui nyingi ambazo zinafaa kwa rejea kwa wadau wa sheria nchini huku wananchi wakihimizwa kukisoma, kwani watajifunza mambo mengi ambayo yamefanyika chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ikiwemo mageuzi na maboresho makubwa katika sekta ya sheria.

Pia, ametumia nafasi hiyo kuwahimiza Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano nchini, kwani bila amani hakuna maendeleo na uchumi endelevu.
Naibu Waziri Katimba
Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,Mheshimiwa Zainab Katimba amesema, kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia kina mchango muhimu katika taaluma ya sheria na uongozi na kinadhihirisha namna uongozi wa Rais Samia ulivyoendelea kuimarisha misingi ya utawala wa sheria, haki, uwajibikaji, maridhiano, ushirikishwaji wa wananchi na maendeleo jumuishi.
Amesema, ni jambo la kujivunia kuona wataalam wakitumia taaluma zao kufanya tafakuri na uchambuzi unaochangia kujenga hazina ya maarifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, amesema Wizara ya Katiba na sheria inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, elimu ya sheria na huduma za msaada wa kisheria kupitia Msaada wa Kisheria wa Mama Samia Awamu ya Pili.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari amesema, kitabu hicho hakikuandikwa kwa lengo la kusifu Serikali au viongozi, bali ni kazi ya kitaaluma inayochambua kwa ushahidi namna sheria,sera na taasisi zilivyotumika kuleta mabadiliko tangu Machi mwaka 2021.
Ameeleza kuwa, wazo la kuandika kitabu hicho lilitokana na tafakari kuhusu nafasi ya sheria katika maendeleo ya taifa, ambapo waandishi walitaka kujibu maswali muhimu kuhusu namna marekebisho ya sheria, maboresho ya sera na uimarishaji wa taasisi za umma vilivyochangia matokeo chanya katika uchumi na ustawi wa jamii.


"Kitabu hiki hakikuandikwa kama maandiko ya sifa, bali ni kazi ya uchambuzi wa kitaaluma inayotumia ushahidi, takwimu na nyaraka rasmi kuchunguza kama mageuzi ya kisheria na kisera yaliyofanyika tangu mwaka 2021 yanaonesha mfumo unaoweza kueleweka, kupimwa na kujadiliwa kitaaluma," alisema Johari.
Amebainisha kuwa, lengo kuu la waandishi lilikuwa kuhamisha mjadala kutoka katika kauli za jumla kwenda kwenye tathmini inayotegemea ushahidi wa kisayansi kuhusu matokeo halisi ya marekebisho ya sheria na sera kwa wananchi.
Sheria kama injini ya maendeleo
Mheshimiwa Johari amesema, kitabu kinaonesha wazi kuwa katika kipindi cha Awamu ya Sita kumekuwa na mwelekeo mpya wa kutumia sheria, sera, taasisi na mifumo ya utekelezaji kujenga mazingira yanayochochea maridhiano, uwekezaji, uwazi, haki, utoaji wa huduma bora na maendeleo ya wananchi.
Amesema, mageuzi hayo yameonekana katika sekta mbalimbali ikiwemo kodi na mapato, uwekezaji, nishati, ardhi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), utalii, elimu, msaada wa kisheria, hifadhi ya jamii, utawala bora pamoja na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Pia,amesema kutokana na umuhimu wa mwelekeo huo, waandishi waliona ni vyema kuuandika na kuuacha kama rejea kwa watunga sera, watafiti, wasomi, mawakili na wadau wengine wanaotaka kuelewa nafasi ya sheria katika maendeleo ya taifa.


Ameeleza kuwa, sheria bora zinapaswa kuwa wazi, zenye mantiki, zinazotekelezeka na zinazotabirika, huku zikiweka mazingira rafiki kwa ukuaji wa uchumi na uimarishaji wa taasisi za umma.
Aidha, ameonya kuwa sheria zenye utata zinaweza kuchelewesha maendeleo, kuongeza migogoro na kukwamisha biashara pamoja na uwekezaji, wakati sheria dhaifu zinaweza kufungua mianya ya matumizi mabaya ya madaraka na upotevu wa rasilimali za taifa.
Waandishi na wahakiki wabobezi
Mheshimiwa Johari amesema, kazi ya uandishi wa kitabu hicho iliongozwa na Profesa Ambrose T. Kessy kwa kushirikiana na timu ya mawakili waliokusanya taarifa, kuchambua sheria, sera na takwimu mbalimbali kabla ya kuandaa uchambuzi huo.
Ameongeza kuwa, kitabu kilihakikiwa na wataalamu waliobobea katika taaluma za sheria, uchumi, sayansi ya siasa na utawala wa umma ili kuhakikisha kinafikia viwango vya juu vya kitaaluma na kuzingatia ushahidi badala ya maelezo yasiyo na msingi.Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maandalizi ya kitabu yalitumia nyaraka rasmi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Wizara ya Elimu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), TANESCO, REA, TCRA, TISEZA, NSSF pamoja na taasisi nyingine.
Aidha, baadhi ya taarifa kutoka Benki ya Dunia (World Bank), UNCTAD na World Travel and Tourism Council (WTTC) zilitumika kuweka muktadha wa kimataifa, huku msingi mkuu wa uchambuzi ukiwa taarifa rasmi za Tanzania.
Sekta nyingi zajadiliwa
Johari amesema, kitabu hicho kinachambua kwa kina sekta mbalimbali zikiwemo elimu, kodi na mapato, uwekezaji, nishati, TEHAMA, ardhi, utalii, hifadhi ya jamii, msaada wa kisheria, utawala bora, usawa wa kijinsia, matumizi ya fedha za UVIKO-19 na nafasi ya sheria katika maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa,hoja kuu ya kitabu hicho ni kwamba sheria zinapaswa kupimwa kwa matokeo yake kwa wananchi badala ya kupimwa kwa idadi ya sheria zilizotungwa.
"Haitoshi kusema sheria imetungwa. Lazima tujiulize imeongeza nini, imeboresha nini, imeondoa kikwazo gani, imeongeza haki kiasi gani na imewafikia wananchi wangapi,"amesema.
Ameongeza kuwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kusimamia ubora wa utungaji wa sheria, usimamizi wa mikataba ya Serikali, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma za kisheria pamoja na kujenga uwezo wa mawakili wa Serikali ili waendane na mabadiliko ya uchumi, teknolojia na mazingira ya kimataifa.
Johari pia amesema,kitabu hakijafumbia macho changamoto zilizopo, zikiwemo uratibu wa taasisi, utekelezaji wa baadhi ya sheria, migogoro ya ardhi, mzigo wa kodi kwa baadhi ya makundi, changamoto za TEHAMA pamoja na tofauti za maendeleo kati ya maeneo ya mijini na vijijini.
Kutokana na hali hiyo, amesema kitabu kinapendekeza kuanzishwa kwa mfumo endelevu wa ufuatiliaji na tathmini ya sheria na sera ili kupima athari zake katika maendeleo ya taifa baada ya kipindi cha utekelezaji.
UDSM: Serikali imewekeza katika maarifa








Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William-Andey Lazaro Anangisye amesema,uzinduzi wa kitabu hicho unaonesha namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyothamini maarifa, tafiti na machapisho ya kitaaluma kama nyenzo za maendeleo ya taifa.
Amesema,Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, hususan elimu ya juu, jambo lililosaidia kuimarisha uzalishaji wa maarifa yanayochangia maendeleo ya nchi.
Profesa Anangisye ameahidi kuwa,UDSM itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuendeleza tafiti na machapisho yatakayosaidia kukuza taaluma mbalimbali, ikiwemo sheria.
Chama cha Mawakili wa Serikali
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Wakili Bavoo Junusi amesema,wazo la kuandika kitabu hicho lilizaliwa Juni 21, 2025 wakati wa Kongamano la Kitaifa la Kisheria baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupendekeza kuandaliwa kwa andiko litakalochambua nafasi ya sheria katika maendeleo.
Amesema, kitabu kimepewa jina la Rais Dkt. Samia kutokana na namna ambavyo Serikali yake imeendelea kutekeleza falsafa ya 4R – Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga Upya (Rebuilding) ambayo imeleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali, hususan sheria.
Aidha, amesema kitabu kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwapa wananchi wengi zaidi fursa ya kukisoma na kushiriki katika mijadala kuhusu mchango wa sheria katika maendeleo ya taifa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Wakili Addo November amesema, kitabu kinaelezea kwa kina mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwaka 2021 na namna yalivyosaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha uchumi.Amesema,pia kitabu kinaangazia mafanikio ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), ambayo hadi sasa imewanufaisha zaidi ya Watanzania milioni nane kwa kuwapatia elimu na msaada wa kisheria bila malipo.
Kwa mujibu wa viongozi hao, kitabu hicho kinatarajiwa kuwa rejea muhimu kwa Serikali, vyuo vikuu, watafiti, mawakili, sekta binafsi na wadau wengine katika kuendeleza mjadala kuhusu nafasi ya sheria kama msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.