NA DIRAMAKINI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Meru iliyopo mkoani Arusha, ni miongoni mwa wilaya zenye ukuaji wa kasi nchini kutokana na mchanganyiko wa shughuli za kilimo, ufugaji, biashara, utalii na uwekezaji. Ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mtandao mpana wa vijiji na mitaa unaorahisisha utoaji wa huduma za kijamii na kusogeza maendeleo karibu na wananchi.
Kwa sasa, Wilaya ya Meru ina jumla ya vijiji 90 vilivyopangwa katika kata mbalimbali, huku baadhi ya maeneo ya mijini yakijumuisha mitaa inayorahisisha usimamizi wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma za Serikali.
Kata ya Usa River, ambayo ni moja ya maeneo yenye shughuli nyingi za biashara na makazi, ina mitaa tisa ambayo ni Usa Madukani, Ngaresero, Mji Mwema, Kwa Kisambare, Magadirisho, Mlima Sayuni, Magadini, Manyata Kati na Nganana.
Eneo hilo limeendelea kukua kutokana na uwepo wa miundombinu ya usafiri, biashara na huduma mbalimbali za kijamii.
Kata ya Maji ya Chai inajumuisha vijiji vya Maji ya Chai, Ngurdoto, Kitefu na Lerai, huku Nkoaranga ikiwa na vijiji vya Nkoaranga, Nshupu na Ngyani. Maeneo hayo yanajulikana kwa shughuli za kilimo, hasa cha mazao ya biashara na chakula, pamoja na ufugaji.
Katika Kata ya Poli kuna vijiji vya Poli, Ndatu na Njoro, wakati Seela Sing'isi inaundwa na vijiji vya Seela, Sing'isi na Malala. Aidha, Kata ya Akheri ina vijiji vya Akheri, Patandi na Nguruma, vinavyoendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.
Kata ya Nkoarisambu inajumuisha vijiji vya Nkoarisambu, Mfulony na Kimundo, huku Nkoanrua ikiwa na vijiji vya Nkoanrua, Loita Nkoamala na Kipande Nkoavele.
Kata ya Songoro ni miongoni mwa kata zenye idadi kubwa ya vijiji, ikiwa na Songoro, Sura, Ushili, Urisho, Mulala na Kilinga, wakati Ngarenanyuki inaundwa na vijiji vya Olkung'wado na Ilkirimuny.
Katika Kata ya Kikwe kuna vijiji vya Kikwe, Nambala, Maweni na Karangai, huku Mbuguni ikiwa na vijiji vya Mbuguni, Mikungani na Kikuletwa. Kata ya Makiba inajumuisha vijiji vya Makiba, Valeska, Patanumbe na Majengo.
Kata ya Marorony ina vijiji vya Marorony, Samaria, Kwaugoro na Migandini, wakati Kikatiti ina vijiji vya Kikatiti, Nasholi, Sakila Chini, Ngyeku na Sakila.
Kwa upande wa Kata ya King'ori, ambayo ni moja ya kata kubwa wilayani humo, inaundwa na vijiji vya King'ori, Mareu, Nkoansiyo, Nsengony, Nkoanoeli, Mboreny, Muungano na Oldonyongiro.
Aidha, Kata ya Leguruki ina vijiji vya Leguruki, Nkoasenga, Miririny na Kandashe, huku Shambarai Burka ikiwa na vijiji vya Shambarai Burka, Kerikeni, Msitu wa Mbogo na Kambi ya Tanga Juu.
Kata ya Majengo inajumuisha vijiji vya Majengo Kati, Kaloleni na Engatani, wakati Malula ina vijiji vya Kolila, Ngejisosia na Nrumangeny.
Katika Kata ya Uviro kuna vijiji vya Uviro, Kisimiri Juu na Kisimiri Chini, huku Ngabobo ikiwa na vijiji vya Ngabobo, Oltepes na Tenki.
Kata ya Maruvango inaundwa na vijiji vya Maruvango, Shishitony, Mbaaseny na Mouwara, wakati Imbaseny ina vijiji vya Imbaseny, Ngongongare na Kiwawa.
Kwa upande wa Kata ya Ambureni, kuna vijiji vya Ambureni na Shangarai, huku Kata ya Nkoanekoli ikijumuisha vijiji vya Nkoanekoli, Nkure na Sangananu.
Mtandao huu wa vijiji na mitaa umeendelea kuwa msingi muhimu wa utekelezaji wa shughuli za Serikali katika ngazi ya msingi, zikiwemo utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, kilimo, barabara na maendeleo ya jamii.
Kupitia mgawanyo huo wa kiutawala, Wilaya ya Meru imeendelea kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, sambamba na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Hali hiyo imechangia kuimarika kwa utawala bora, kuongeza uwajibikaji wa viongozi wa maeneo husika na kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Kadri idadi ya watu na shughuli za kiuchumi zinavyoendelea kuongezeka, vijiji na kata za Wilaya ya Meru vinatarajiwa kuendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa eneo hilo pamoja na Taifa kwa ujumla.
