Serikali yampongeza mwanafunzi mwenye mahitaji maalumu,Biriati Yafet kwa kuongoza Matokeo ya Kidato cha Sita 2026

RUVUMA-Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameongoza hafla ya kumpongeza mwanafunzi Biriati Yafet mwenye mahitaji maalum na anayetokea katika mazingira magumu, baada ya kupata Daraja la Kwanza (Division I) kwa pointi 3 kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka 2026.
Katika hafla ya pongezi, Brigedia Jenerali Ahmed amesema tukio hilo liwe hamasa kwa wanafunzi wengine katika mkoa kusoma kwa bidii na kupata ufaulu wa juu. Amesema Biriati Yafet atatunukiwa zawadi ya shilingi milioni tatu na kusisitiza kuwa ataendelea kumfuatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha anafikia malengo yake.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi wa elimu na jamii kuimarisha juhudi za kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum na wanaotokea katika mazingira magumu, akitolea mfano mchango wa Kalamu Education Foundation katika kumsaidia Biriati.

Kwa upande wake, Biriati Yafet, amesema mafanikio yake yametokana na nidhamu na bidii katika kusoma. Ameongeza kuwa ndoto yake kubwa ni kusoma nje ya nchi hivyo ameiomba serikali pamoja na mashirika mbalimbali kumsaidia kufanikisha malengo hayo, kwani anaamini atafanya vizuri sana.

Kwa upande mwingine, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Louis Chomboko, amesema mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu kwa wanafunzi wengine kuongeza bidi katika masomo.

Naye Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mwl. Mathias Tilia, amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi kama biriati ili waweze kupata elimu bora na kufikia malengo yao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kalamu Foundation, Said Bwanaally, amesema lengo lao ni kuwapa matumaini wanafunzi wenye mahitaji maalum na wanaotokea katika mazingira magumu wajione wana uwezo wa kusoma na kufikia malengo yao.

Biriati Yafet Biriati ni mzaliwa wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. Alisoma Shule ya Msingi Imani kata ya Lukumbule, kisha Songea Boys kwa kidato cha kwanza hadi cha nne, na Ndanda Boys kwa kidato cha tano na sita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here