NA DIRAMAKINI
ZAIDI ya nusu ya watu wanaofanya kazi nchini Namibia wanalazimika kukopa fedha ili kununua chakula cha kila siku, hali inayodhihirisha kuongezeka kwa changamoto za kiuchumi na gharama za maisha nchini humo.
Takwimu za Wakala wa Takwimu wa Namibia (Namibia Statistics Agency-NSA) zinaonesha kuwa asilimia 51.3 ya watu wanaofanya kazi na wanaotumia mikopo hutegemea fedha za kukopa ili kugharamia mahitaji ya msingi ya chakula.
Hali hiyo imeibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa gharama za maisha, huku ajira rasmi zikiwa hazitoshi tena kuhakikisha baadhi ya wafanyakazi wanapata usalama wa chakula na mahitaji mengine muhimu ya kila siku.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, mahitaji ya msingi ya maisha ndiyo yanayoongoza katika matumizi ya mikopo nchini Namibia, badala ya mikopo kutumika zaidi kwa uwekezaji au ununuzi wa mali zinazoweza kuongeza kipato.
Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia 51.3 ya wakopaji wanaotoka katika kundi la watu wanaofanya kazi hutumia mikopo kununua chakula, wakati asilimia 22.1 hukopa kugharamia elimu, ikiwemo ada za shule na mahitaji ya kujifunzia.
Aidha, asilimia 16.4 ya wakopaji hutumia mikopo kugharamia usafiri wa kila siku wa kwenda na kurudi kazini.
Kwa ujumla, ushiriki wa watu wazima katika mikopo umeendelea kuongezeka nchini humo. Takwimu zinaonesha kuwa, kiwango cha watu wazima wanaokopa kiliongezeka kutoka asilimia 42.1 mwaka 2017 hadi asilimia 49.0 mwaka 2025.
Wachambuzi wa uchumi wanasema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kutokuwiana kati ya mishahara na ongezeko la gharama za maisha.
Takribani asilimia 54 ya wafanyakazi 546,000 nchini Namibia wanakadiriwa kupata chini ya dola za Namibia 2,000 kwa mwezi, hali inayowaweka katika mazingira magumu ya kukabiliana na ongezeko la bei za bidhaa na huduma muhimu.
Wataalamu wa masuala ya fedha wanaonya kuwa,matumizi ya mikopo kununua bidhaa zisizodumu, hususan chakula ni ishara ya changamoto kubwa ya kiuchumi kwa kaya.
Wanasema tofauti na mikopo inayotumika kununua nyumba, kuanzisha biashara au kufanya uwekezaji unaoweza kuzalisha kipato, kukopa kwa ajili ya matumizi ya kila siku hakutengenezi mali wala chanzo cha mapato ya baadaye.
Badala yake, hali hiyo inaweza kuwaweka watu wenye kipato cha chini katika mzunguko wa madeni, ambapo wanakopa ili kukidhi mahitaji ya sasa na baadaye kulazimika kutumia sehemu kubwa ya kipato chao kulipa madeni na riba.
Kwa mujibu wa wachambuzi, kuongezeka kwa utegemezi wa mikopo kwa ajili ya chakula ni ishara kwamba changamoto za gharama za maisha nchini Namibia zimefikia hatua inayohitaji hatua za kiuchumi zinazolenga kuongeza kipato cha kaya, kudhibiti mfumuko wa bei na kuboresha uwezo wa wananchi kumudu mahitaji ya msingi.
Hali hiyo pia imeibua mjadala kuhusu umuhimu wa sera zinazolenga kuongeza mishahara, kupanua fursa za ajira zenye kipato cha kutosha na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa kijamii kwa kaya zenye kipato cha chini.
Pia,wataalamu wanaonya kuwa endapo mishahara itaendelea kubaki chini wakati gharama za chakula, usafiri na elimu zikiongezeka, idadi ya wananchi watakaolazimika kukopa ili kukidhi mahitaji ya msingi inaweza kuendelea kuongezeka.
Kwa hiyo, takwimu hizo zinaonesha changamoto pana zaidi ya madeni ya mtu mmoja mmoja, zikielekeza kwenye hitaji la kuchukua hatua za kimuundo ili kuhakikisha ajira na mishahara vinawawezesha wananchi kumudu maisha bila kulazimika kutegemea mikopo kwa ajili ya chakula cha kila siku.
