LINDI-Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limefanya mazoezi ya kutembea (Route March) ikiwa ni moja ya sehemu ya mazoezi kwa Askari Polisi kwa lengo la kujenga utimamu wa mwili, kukimbiza magonjwa nyemelezi pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.
Mazoezi hayo yalianzia Bwalo la Maafisa wa Polisi Mkoa wa Lindi kuelekea mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Lindi na kutamatika kwenye uwanja wa Mpira wa Kikapu wa "SEA VIEW" kwa kufanya mazoezi mbalimbali ya viungo ambayo yaliongozwa na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Andrew Ngassa.
Aidha,ACP Ngassa amesema kuwa mazoezi haya ni muhimu kwa Askari wote na hufanyika kila siku kwenye vikosi vya kijeshi na wilaya zote za Mkoa wa Lindi ingawa kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi hukutana kwa pamoja na kufanya mazoezi hayo huku akiwasisitiza Askari hao kufanya kazi kwa kuzingatia kaulimbiu ya Jeshi la Polisi isemayo, "Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu ni Msingi wa Mafanikio Yetu".






