Rais Dkt.Mwinyi kumwakilisha Rais Dkt.Samia katika Kumbukumbu ya Miaka 65 ya Mkutano wa Kwanza wa NAM nchini Serbia

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuelekea Jamhuri ya Serbia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Kumbukumbu ya Miaka 65 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NON-ALIGNED MOVEMENT-NAM) jijini Belgrade, Serbia.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 29,2026 na Raqey Mohamed ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi, akiambatana na ujumbe wake, atashiriki maadhimisho hayo yatakayofanyika tarehe 31 Agosti hadi 01 Septemba 2026 katika Kasri la Serbia, jijini Belgrade.

Mkutano huo unalenga kutafakari historia na urithi wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote, pamoja na umuhimu wa misingi yake katika mazingira ya sasa ya kisiasa na kiuchumi duniani. Tanzania inatarajiwa pia kuwasilisha taarifa yake katika kikao cha Mkutano huo.

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri waliotoa mchango mkubwa katika kuendeleza misingi na malengo ya Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), hususan katika kutetea uhuru wa mataifa, kujitawala, usawa, amani, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa.

Mkutano wa kwanza wa Wakuu wa Nchi wa NAM ulifanyika Belgrade mwaka 1961, ukiweka msingi wa Harakati hizo ambazo zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la ushirikiano wa mataifa mbalimbali.

Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Aleksandar Vučić, ambapo atawasilisha Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Viongozi hao wanatarajiwa kujadili uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Serbia, hususan katika maeneo ya biashara na Uwekezaji, Kilimo, Utalii na Uchumi wa Buluu pamoja na maeneo mengine yenye maslahi kwa pande zote.

Rais Dkt. Mwinyi pia anatarajiwa kushiriki mazungumzo na wawekezaji wa Serbia ikiwa ni sehemu ya kuendeleza fursa za biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Ziara ya Rais Dkt. Mwinyi nchini Serbia inatarajiwa kukamilika tarehe 02 Septemba 2026, baada ya kushiriki Mkutano huo pamoja na shughuli nyingine zilizopangwa pembezoni mwa maadhimisho hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here