Balozi Yakubu ahimiza Watanzania kutembelea Kituo cha Michoro ya Miambani Kondoa

DODOMA-Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Mhe. Saidi Othman Yakubu amewahimiza Watanzania kutembelea Kituo cha Michoro ya Miambani cha Kondoa mkoani Dodoma ili kujifunza historia, utamaduni na urithi mkubwa unaopatikana katika eneo hilo.
Balozi Yakubu ametoa wito huo wakati wa ziara yake katika Kituo hicho, ambayo imelenga kujionea hali ya uhifadhi wa eneo hilo la Urithi wa Dunia na kutathmini ushirikiano uliopo kati ya wasimamizi wa Kituo, Serikali ya Tanzania na UNESCO.

Amesema, Michoro ya Miambani ya Kondoa ni ushahidi muhimu wa historia ya maisha, shughuli, imani na ubunifu wa jamii zilizoishi katika eneo hilo kwa vizazi mbalimbali. Hivyo, Watanzania wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuutambua, kuuthamini na kuulinda urithi huo.

“Ni muhimu Watanzania tutembelee maeneo yetu ya Urithi wa Dunia. Kwa kufanya hivyo, tunajifunza historia yetu, tunakuza uzalendo, tunaunga mkono juhudi za uhifadhi na pia tunachangia kukuza utalii wa ndani pamoja na uchumi wa jamii zinazozunguka maeneo haya,” amesema Balozi Yakubu.
Katika ziara hiyo, Balozi Yakubu ameambatana na Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Dkt. Khamis Khalid Said, pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Ujumbe huo umepokea maelezo kuhusu historia na umuhimu wa michoro hiyo, hatua zinazochukuliwa katika usimamizi na uhifadhi wake, pamoja na changamoto na fursa zilizopo katika kuendeleza eneo hilo kama kivutio muhimu cha urithi na utalii.

Balozi Yakubu amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania na wadau wengine katika kulinda eneo hilo.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa jamii zinazozunguka Kituo, elimu kwa vijana, utafiti, miundombinu ya wageni na matumizi ya teknolojia katika kutangaza na kuhifadhi michoro hiyo.

Ametoa shukrani kwa Mkuu wa Kituo cha Michoro ya Miambani Kondoa, Bw. Zuberi Mabie, Mkuu wa TFS Kanda ya Kati, Bw. Ignatius Lupala, pamoja na watumishi wote wa Kituo kwa mapokezi yao na kazi wanayoifanya katika kulinda urithi huo muhimu.

Kwa upande wake, Dkt. Khamis Khalid Said amesema, Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania itaendelea kushirikiana na taasisi husika katika kuimarisha uhifadhi, elimu, utafiti na uhamasishaji kuhusu maeneo ya Urithi wa Dunia nchini.
Michoro ya Miambani ya Kondoa ni miongoni mwa maeneo saba ya Tanzania yaliyoorodheshwa katika Orodha ya Urithi wa Dunia ya UNESCO. Eneo hilo lina mkusanyiko mkubwa wa michoro ya kale inayotoa ushahidi muhimu kuhusu maisha na mabadiliko ya jamii zilizowahi kuishi katika eneo la kati la Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here